Pages

Wednesday, December 31, 2014

MKAKATI KUHAMASISHA UTALII WA NDANI WAANZA KULETA TIJA

Mkuu wa Idara ya Utalii ya Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, Eva Mallya.
Mkakati endelevu wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) wa kuhamasisha utalii wa ndani unaolenga kuongeza idadi ya Watanzania kutembelea hifadhi mbalimbali nchini, umeanza kuleta tija.
Hali hiyo imekuja baada ya Taasisi na Kampuni ya Sekta Binafsi kufungua fursa hiyo kwa wafanyakazi wake kuona na kujivunia maliasili na rasilimali walizonazo kama taifa. Mkuu wa Idara ya Utalii ya Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, Eva Mallya, alisema licha ya Tanzania kuzidi kung’ara kwenye sekta hiyo Barani Afrika kutokana na ubora na wingi wa vivutio vyake, mwamko wa Watanzania kama watalii wa ndani umeanza kuleta matumaini.
Eva alikuwa akizungumza jana na watumishi wa Kampuni ya Uwekezaji ya Marenga ya mjini Moshi, waliofanikiwa kuitembelea hifadhi hiyo na kisha kupanda Mlima Kilimanjaro kupitia lango la Londorosi Wilaya ya Siha, wakiwa wameishia mita 3,700 kutoka usawa wa bahari.
“Mkakati wa kukuza utalii wa ndani, unaanza kuleta matumaini hasa kwenu nyie ambao mmefanya uamuzi mzuri wa kutembelea na kupanda Mlima Kilimanjaro, ingawa kiuhalisia mwamko bado ni mdogo…katika wageni 51,000 waliotembelea hifadhi za taifa kwa mwaka wa fedha uliopita, asilimia 95 ya watalii, walikuwa wageni kutoka nje ya nchi na asilimia tano ni wa ndani,” alisema.
Kwa mujibu wa mhifadhi huyo, bado kuna changamoto ya watalii wa ndani kutembelea hifadhi zilizopo hapa nchini ukilinganisha na watalii kutoka nje ya nchi. Aidha, alisema jitihada za makusudi zinahitajika kuwahamasisha Watanzania kuona umuhimu wa kutembelea vivutio hivyo, licha ya ukweli kwamba tayari Tanapa ilikwisha punguza gharama za kutembelea vivutio hivyo kwa watalii wa ndani.
Hata hivyo, Joseph Kimoso, ambaye ni Mkurugenzi wa Marenga, alisema licha ya hifadhi hiyo ya Kilimanjaro kutangazwa kuwa moja ya Maajabu Saba ya Dunia, bado Watanzania hawajaelimishwa vya kutosha kuhusu umuhimu wa kutembelea hifadhi na vivutio.
Badala yake, aliitaka Tanapa kuanzisha klabu maalum za utalii katika shule za msingi, sekondari na vyuo kwa lengo la kuongeza hamasa kwa watalii wa ndani. Kwa upande wake, Edson Lekei, alitoa rai kwa kampuni, taasisi na vyuo vilivyopo mkoani Kilimanjaro na mikoa ya jirani, kujiwekea utaratibu wa kuwahamasisha na kuwahimiza watumishi wao kuitembelea Hifadhi ya Kinapa nyakati za mapumziko ya sikukuu za kitaifa badala ya kuwaandalia sherehe ambazo huishia kufanya anasa za kula na kunywa. Utalii mwingine katika hifadhi hiyo ni pamoja na vivutio vya wanyama kama tembo, chui, nyati, simba na makundi mbalimbali ya ndege wa aina mbalimbali.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment