Social Icons

Pages

Wednesday, December 24, 2014

MACHINGA DAR WAFUNGA MITAA, MABOMU YATANDA

Mama Lishe wakimbeba mwenzao aliyepoteza fahamu kutokana na mabomu ya machozi yaliyopigwa na polisi eneo la Kariakoo kuwaondoa wamachinga jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni gari mojawapo la polisi katika operesheni hiyo.
Milio ya risasi zilizokuwa zikifyatuliwa na askari wa Jeshi la Polisi jana ilirindima katika Soko Kuu la Kariakoo, jijini Dar es Salaam na kuzua taharuki kubwa kwa wafanyabiashara, wateja pamoja na wapita njia katika eneo hilo.
Hali hiyo ilizuka baada ya wafanyabiashara ndogo ndogo, maarufu kama ‘Wamachinga’, kufunga mtaa na kupambana na askari wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Risasi zilizotumika zimeelezwa kuwa ni za moto ambazo zilikuwa zikirushwa hewani na askari hao sambamba na mabomu ya machozi kuwatawanya wamachinga hao.
Wamachinga hao walianzisha mapambano hayo kupinga kuondolewa na askari hao wa jiji kufanya biashara kando kando ya soko hilo. Milio hiyo ya risasi pamoja na mabomu ya machozi, vilisababisha wafanyabishara na wateja katika soko hilo kupatwa na mshtuko na kuanza kukimbia hovyo, wengine kuzimia na wengine kupata majeraha na kukimbizwa katika vituo vya afya.
Vurugu hizo ambazo zilienea katika mitaa ya Kongo, Msimbazi na Kamata, ilisababisha wafanyabishara kufunga maduka kwa muda ili kunusuru maisha yao na mali zao. Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, ambaye ni mfanyabishara wa duka, Saraphina Kessy, alisema saa 6:00 mchana alishuhudia askari wa Jiji pamoja na wa jeshi hilo wakipita karibu na duka lake wakiwa na silaha.
Alisema muda mfupi baadaye, magari yaliyowabeba askari wengine, wakiwa na silaha,  yalielekea upande wa mtaa wa Msimbazi kabla ya kuanza kufyatua risasi hizo. “Kwa kweli tulishtuka kutokana na milio ya risasi iliyotanda kila kona. Watu wakaanza kukimbia hovyo. Wateja waliokuwa wakipita wakaanza kuingia kwenye maduka ya watu kutafuta hifadhi. Kwa hiyo, kukawa hakuna usalama kiasi cha watu kulazimika kufunga maduka yao,” alisema Saraphina.
Flora Shirima, alisema askari hao, ambao walikuwa wakilumbana na madereva wa pikipiki, maarufu kama bodaboda mtaa wa Msimbazi, walianza kurusha mabomu ya machozi yaliyotawanya watu, ambao walianza kukimbia hovyo na kusababisha madhara. Alisema hali hiyo ilisababisha baadhi ya watu kukimbia hovyo na kukanyagana, wengine kuibiwa na maduka mengi kufungwa kwa kuhofia kuibiwa kutokana na vurugu hizo.
“Ninavyoongea na wewe hapa, ndiyo ninafungua duka langu. Hiki kitendo cha Jeshi la Polisi kupiga mabomu katika msongamano mkubwa wa watu kiasi hiki ni cha hatari. Kuna watu wameumia sana na wengine wamepata mshtuko. Lazima wajali usalama wa watu kwanza,” alisema Flora.
NIPASHE ilizungumza na Prisca Mushi, ambaye ni muuguzi wa zahanati ya Front Line, ambako baadhi ya majeruhi wa tukio hilo walipelekwa kupata matibabu. Prisca alithibitisha kupokea majeruhi wanne katika zahanati hiyo na kusema wawili kati yao walikuwa wanawake, ambao walipata mshtuko kutokana na mabomu hayo, akiwamo mjamzito mmoja. “Hawa wanawake wawili, mmoja alikuwa mjamzito. Tuliwapatia matibabu ya dharura, ikiwamo kuwachoma sindano na kuwatundikia dripu na kuwapumzisha kwa muda, kwani walipatwa tu na mshtuko na baadaye tuliwaruhusu,” alisema Prisca. Alisema wengine walikuwa ni wanaume wawili, ambao walikuwa wamepatwa na majeraha katika sehemu mbalimbali za miili yao, hivyo wote walipewa huduma ya kwanza na kuruhusiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema wanawashikilia watu 24 kwa tuhuma za kuhusika na vurugu hizo. Alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 6:00 mchana wakati askari wa jiji walipokuwa wakiwaondoa wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara kando kando ya barabara katika soko hilo.
Kamanda Nzuki alisema wamachinga hao, ambao walikuwa wakifanyabishara barabarani, walizuiwa na askari wa jiji, lakini waligoma kuondoka na kuanza kufanya vurugu. Alisema wafanyabiashara hao waliamua kufanya vurugu kwa kufunga barabara pamoja na kuchoma matairi karibu na ofisi za jiji la Dar es Salaam wakipinga kufukuzwa eneo hilo.
Kamanda Nzuki alisema walilazimika kutumia mabomu ya machozi, risasi za moto zilizofyatuliwa hewani na risasi za vishindo ili kuwatawanya wamachinga hao. “Tulitumia mabomu ya machozi, risasi za vishindo na risasi za moto za hewani ili kuwatawanya wamachinga hao waliokuwa wametawala na kufunga barabara. Tulifanikiwa kuwatawanya na kutuliza ghasia zilizokuwa eneo la tukio. Hakuna aliyeumia,” alisema Kamanda Nzuki.
Alisema watu 24 walikamatwa katika tukio hilo na wanashikiliwa kwa upelelezi zaidi na hatua zaidi zitachukuliwa mara baada ya uchunguzi kukamilika. Tukio hilo limekuja siku moja kabla ya kuadhimishwa kwa sikukuu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, ya Krismasi. Katika kipindi hiki, watu wengi hufika katika soko hilo kupata bidhaa mbalimbali, vikiwamo vyakula na malazi.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: