Social Icons

Pages

Wednesday, December 17, 2014

LIPUMBA ASEMA PINDA NI MZIGO MZITO

 
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba (katikati), akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho, Buguruni jijini Dar es Salaam jana.
Shinikizo dhidi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, limepamba moto baada ya safari hii Chama cha Wananchi (CUF) kumtaka Rais Jakaya Kikwete amwajibishe ili kuepuka kumaliza vibaya kipindi chake cha pili cha uongozi, kwa madai kwamba, amekuwa mzigo mzito kwa serikali.
Tuhuma na shinikizo dhidi ya Pinda linatokana na kuvurugika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Jumapili iliyopita nchini kote.Tamko hilo la CUF lilitolewa na Mwenyekiti wake, Prof. Ibrahim Lipumba, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, juu ya hali ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji katika zoezi la upigaji kura na baada ya matokeo.
CUF ilitoa tamko hilo ikiwa ni siku moja baada ya wenzao wa Chadema kupitia Naibu Katibu Mkuu wake Tanzania Bara, John Mnyika, kumtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia na Pinda (pichani) kutokwepa lawama na rai za kutakiwa kuwajibika kutokana na kasoro ambazo zimejitokeza kwenye uchaguzi huo.
Mbali na Pinda, CUF katika tamko hilo, wanamtaka Rais Kikwete pia kumwajibisha Waziri Ghasia kwa madai ya kushindwa kusimamia vizuri uchaguzi huo.Tayari Waziri Ghasia juzi aliwaambia waandishi wa habari kuwa iwapo uzembe utabainika kufanywa na yeyote kwa sababu yake, atawajibika.
CUF pia wanamtaka Rais Kikwete kuwaachisha kazi wakurugenzi wote waliopewa fungu la fedha kwa ajili ya matumizi ya maandalizi ya uchaguzi kisha wakashindwa kulifanyia kazi kama ilivyokusudiwa na kusababisha usumbufu kwa raia.
Prof. Lipumba alisema wananchi wamechoka na ufisadi aliouita ‘wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)’, unaofanyika kwenye uchaguzi na kwenye mali za umma, kama ule wa uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 uliofanyika katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Alisema kazi kubwa iliyopo ni kuwahamasisha wananchi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura na kujipanga kulinda kura wakati wa uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba, 2015. Hivyo, akasema Rais Kikwete ana wajibu wa kuhakikisha zoezi la kuandikisha wapigakura linaendeshwa vizuri na uchaguzi mkuu hauwi wa hila na vitimbi kama uchaguzi wa serikali za mitaa. “(Rais Kikwete) awe macho na Waziri Mkuu, Pinda. La sivyo atamaliza kipindi chake cha pili vibaya,” alisema Prof. Lipumba.Alisema Pinda amekuwa mzigo mzito siyo tu kwa maneno, bali kwa vitendo pia. Miongoni mwa kauli za Pinda zilizozua utata na kuzua mjadala mkubwa miongoni mwa wananchi nchini, alizitaja kuwa ni pamoja na ile ya kuviagiza vyombo vya dola, hasa Jeshi la Polisi kuwapiga wananchi na kupuuza utawala bora na wa sheria, ambao ndiyo unaopaswa kutumika kuongoza nchi.
Prof. Lipumba alisema kauli nyingine yenye utata iliyowahi kutolewa na Pinda na hivyo kuthibitisha kwamba, kiongozi huyo ni mzigo, ni ile ya kuagiza wanaowaua watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) nao pia wauawe na hivyo kuiruka mahakama, ambayo ndiyo chombo pekee katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinachotambuliwa na katiba na sheria za nchi kutoa haki. Kauli nyingine tata iliyotolewa na Pinda, Prof. Lipumba alisema ni ile ya kubariki uporaji uliofanywa katika akaunti ya Tegeta Escrow kwa kutamka bungeni kwamba, fedha hizo hazikuwa za umma. Prof. Lipumba alisema zaidi ya hivyo, Pinda ameshindwa kusimamia vizuri uchaguzi huo na hivyo kusababisha kuharibika katika maeneo mengi nchini.
“Pinda ni mzigo tena mzigo mzito sana,” alisema Prof. Lipumba.
Alisema matukio yaliyojiri katika uchaguzi huo na kusababisha kuharibika, yamedhihirisha tamko la CUF lililotolewa mara tu baada ya Pinda kutangaza tarehe ya uchaguzi kuwa serikali imekurupuka haikuwa imejiandaa. Prof. Lipumba alisema matokeo yanaonyesha kuwa, wakurugenzi wa halmashauri badala ya kujikita katika maandalizi ya uchaguzi, walijikita zaidi katika kuitafutia CCM ushindi wa bure kupitia pingamizi na kuengua wagombea wa upinzani kwa vigezo visivyo na msingi na wakati huo huo wakiwatetea wagombea wa chama hicho ambao wana makosa sawa na wagombea wa upinzani au makubwa kupitiliza.
Kutokana na hali hiyo, alisema wanasikitishwa kuona fedha za serikali, ambazo ni kodi za wananchi zinatumika kizembe na kuwatesa wananchi hao hao, ambao ndiyo wenye pesa zao kwa kuwasumbua kwa kuacha shughuli zao ili wakapate haki yao ya kidemokrasia ya kupiga kura.Hata hivyo, alisema wazembe wachache wameshindwa kutekeleza majukumu yao ya maandalizi ya vifaa, tena kwa makusudi, kwani maeneo makubwa yaliyoathirika ni yale ambayo CCM ilikuwa inashindwa. Alisema CUF imesikitishwa na mwenendo mzima uliojitokeza katika zoezi zima la upigaji kura wa uchaguzi huo, ambalo lilisababisha vurugu katika baadhi ya vituo. Aliwapongeza wananchi waliojiandikisha na kushiriki katika uchaguzi na kulaani vikali mbinu chafu zilizotumiwa na CCM na dola kuchakachua uchaguzi huo. Alitaja baadhi ya matukio ya mbinu yaliyojiri katika uchaguzi huo kuwa ni pamoja na wagombea 14 wa nafasi ya uenyekiti wa vijiji na vitongoji katika wilaya ya Lushoto, mkoani Tanga, kuenguliwa siku moja kabla ya uchaguzi. Alisema wagombea hao walikumbwa na mkasa huo kwa madai kwamba walishindwa katika rufaa zilizokatwa dhidi yao, huku wakiwa wameshiriki katika kampeni kwa muda wote.
Hata hivyo, alisema pamoja na vitimbwi vya CCM na dola kuchakachua uchaguzi, kuna maeneo ambayo wananchi wamefanikiwa kulinda kura. Alitoa mfano wilaya ya Kilwa, kata ya Kilwa Kivinje, kuwa CUF imeshinda vijiji 17, huku CCM ikiambulia vijiji sita, ikiwamo kimoja kwa pingamizi.
Alisema katika kata ya Masoko, CUF ilishinda vijiji vitano na CCM vinne kimoja kwa pingamizi; kata ya Somanga (CUF-vijiji vinne) na (CCM kijiji kimoja); kata ya Kinge-Njia nne (CUF kijiji kimoja) na (CCM vijiji viwili); kata ya Micheja (CUF vijiji viwili) na (CCM viwili); kata Chumo (CUF vijiji vitatu) na (CCM vijiji viwili); kata ya Pande (CUF vijiji vitano) na (CCM vijiji viwili) na kata ya Njinjo (CUF vijiji viwili) na (CCM kijiji kimoja). Alisema kata nyingine ni Miguruwe (CUF kijiji kimoja) na (CCM vijiji viwili); kata ya Nanjilinji (CUF vijiji viwili) na (CCM kijiji kimoja); kata ya Mandewa (CUF vijiji vitatu) na (CCM vijiji vitatu, kimoja kikiwa ni kwa pingamizi). Alisema katika Wilaya ya Liwale mjini, mkoani humo, CUF imeshinda vijiji 10 na CCM vijiji vitano kati ya vijiji 15 na kwamba, taarifa kamili zitatolewa na Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF.

HABARI YA KUSIKITISHA
Alisema katika kitongoji cha Mwarongo, kata ya Tongoni, wilaya ya Tanga Mjini, Mwenyekiti aliyeshinda kitongoji hicho kupitia CUF, alifariki dunia saa 9 usiku wakati wa kusherehekea ushindi alioupata, baada ya kuzidiwa na shinikizo la damu Kwa mujibu wa Prof. Lipumba, marehemu enzi za uhai wake, alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa pumu. Alisema matukio ya uchakachuaji wa uchaguzi huo, yanadhihirisha umuhimu wa kutekeleza makubaliano ya vyama vya siasa na Tamisemi yaliyofikiwa Julai 15, mwaka huu, mkoani Morogoro, ikiwamo uchaguzi wa madiwani ufanyike pamoja na uchaguzi wa mitaa na vijiji ili uongozi wote wa serikali za mitaa wachaguliwe kwa wakati mmoja. Pia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) iratibu na kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa, daftari la kudumu la wapigakura litumiwe katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji na mabadiliko ya sheria ya uchaguzi wa serikali za mitaa yafanyike haraka kuzingatia mapendekezo hayo na kuingiza maadili ya uchaguzi wa serikali za mitaa. “Serikali ingeyatekeleza mapendekezo haya uchaguzi wa serikali za mitaa ungesubiri mpaka daftari la wapigakura kukamilishwa,” alisema Prof. Lipumba.
CHANZO: NIPASHE

No comments: