Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika (kulia) akizungumza
kuhusu hali ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika nchi nzima
juzi. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu.
Kamati Kuu ya Chadema, inatarajia kukutana kwa dharura kujadili uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Hatua hiyo inatokana na malalamiko kutoka kwa
wapigakura, wagombea na vyama mbalimbali vya siasa kuhusu kuvurugika na
kutofanyika kwa uchaguzi katika baadhi ya maeneo kutokana na kasoro
mbalimbali. Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika
alisema jana kuwa baada ya hujuma na ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi
huo, kamati kuu itakuja na mapendekezo ya nini cha kufanya. “Kikao hicho kitakuja na maazimio juu ya hatua za
kuchukua dhidi ya Waziri Mkuu (Mizengo Pinda) mwenye dhamana ya Tamisemi
ambao wamevuruga uchaguzi huu. Hata katika maeneo ambayo uchaguzi
umeahirishwa kama Ukawa tutashirikiana kuhakikisha tunaiondoa CCM licha
ya vitendo vya kuhujumu uchaguzi unaofanywa na viongozi wa CCM na wakati
mwingine kwa kulitumia Jeshi la Polisi,” alidai Mnyika.
Ushindi wa Chadema
Kuhusu ushindi wa chama hicho katika uchaguzi huo,
Naibu Katibu Mkuu - Zanzibar, Salum Mwalimu alisema: “Tumefanya vizuri
nchi nzima. Kwa mfano, mwaka 2009 Dar es Salaam yote tulikuwa na mitaa
saba tu lakini leo hii mpaka sasa jimbo moja tu la Ubungo tumeshinda
mitaa 23, unaweza kuona tunavyopiga hatua. “Mwaka 2009, CCM walishinda kwa asilimia 96 na
upinzani tulikuwa tunagawana asilimia nne, sasa leo hii katika maeneo
mbalimbali tumefanya vizuri licha ya hujuma na hila zinazofanywa na CCM.
Baadhi ya maeneo ambayo wanatoka mawaziri, Chadema tumeshinda hivyo
wakitaka kutatuliwa matatizo yao tutawatatulia na tunawaahidi
kuwatumikia vizuri bila upendeleo. “Jimbo la Tundu Lissu la Singida Mashariki ambalo
CCM wamekuwa wakisema watalichukua, kati ya vijiji 43, vijiji 41
tumevichukua na CCM wameambulia viwili, Kyela mwaka 2009, tulikuwa na
mitaa miwili lakini leo tuna mitaa zaidi ya 28.”
Vyama vingine
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema
licha ya uchaguzi huo kutawaliwa na hila na kila aina ya uchakachuaji
wa matokeo, bado vyama vya upinzani vimefanya vizuri.“Ni matokeo mazuri kwa Ukawa licha ya CCM kuwatumia watendaji wa
kata na vijiji kuharibu lakini tumepambana hadi hayo matokeo mnayoona
ni ushirikiano wetu wa Ukawa. Haiwezekani majina ya wagombea wa Ukawa
ndiyo yakosewe halafu ya CCM yawe sawa, kwa nini isiwe wao iwe sisi?
Tunafurahi kuona mikoa ya Kusini (Lindi na Mtwara) tumeongeza vijiji na
mitaa jambo linalotutia moyo,” alisema Profesa Lipumba.
Kuhusu mwingiliano wa wagombea wa Ukawa katika
eneo moja alisema: “Hii ni changamoto ambayo ni lazima tuikubali na
tuifanyie kazi ili katika uchaguzi ujao mwakani isije kujitokeza lakini
kila kitu lazima kiwe na changamoto zake.” Alisema umefika wakati uchaguzi huo ukawa
unasimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kwani baadhi ya matatizo
kama majina ya wahusika kutokuwapo na kuchanganya majina ya wagombea
katika karatasi za kupigia kura yasingetokea.
Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo alisema: “Ni
uchaguzi ambao umeshindwa kufanikiwa kisera na kivifaa hivyo tufike
wakati sasa uchaguzi huu uwe unasimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi
ambao wana mipango ya muda mrefu na si hawa Tamisemi wanaofanya mambo
kwa kukurupuka.”
Katibu Mkuu wa muda wa ACT - Tanzania, Samson
Mwigamba alisema katika Mkoa wa Katavi chama hicho kimefanikiwa kupata
wenyeviti wa vijiji wawili.
Alisema mkoani Kigoma, kimepata wenyeviti wa mitaa tisa, vijiji 10, vitongoji 14 na wajumbe 53.
“Hii ni dalili kwamba upinzani sasa umedhamiria kuiondoa CCM na kama tutajipanga vyema mwakani, CCM inaondoka.” “Bila kubadili uongozi hususan kuitoa CCM
madarakani, basi mabadiliko katika nchi hii tusahau kwani huyo aliyeleta
matatizo hayo anataka kuendelea kung’ang’ania kuongoza,” alisema
Mwigamba. Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP),
Augustine Mrema alisema: “Mpaka sasa nimeshinda vijiji vinane katika
jimbo langu la Vunjo, vitongoji ni vingi ambavyo idadi yake kwa sasa
sina hapa. Wananchi wa Vunjo bado wana imani na mimi kwa kunipa heshima
hiyo... Mrema bado ataendelea kuwa Mbunge wa Vunjo na hao wanaotaka
kuniondoa bado hawana nafasi.”
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema
kukiukwa kwa makubaliano baina ya vyama vya siasa na Serikali ndiyo
kumesababisha yote hayo yaliyotokea. Alisema Septemba 8 mwaka huu, upinzani chini ya
Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ulikutana Ikulu Ndogo Mjini Dodoma
na Rais Jakaya Kikwete na kukubaliana uchaguzi huo usifanyike mwaka huu,
jambo ambalo halikufuatwa.
Alisema walikubaliana uchaguzi ufanyike Machi
mwakani ili kupisha marekebisho ya sheria ya uchaguzi ili uchaguzi huo
usimamiwe na NEC lakini makubaliano hayo yalitupiliwa mbali. “Licha ya upinzani kufanya vizuri lakini tungefanya zaidi ya hapa kama uchaguzi ungesimamiwa na NEC,” alisema Mbatia.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment