Rais Jakaya Kikwete, ametupiwa lawama na makada wa CCM kwa
kusababisha kushindwa CCM viti vingi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa,
kutokana kuchelewa kutoa maamuzi juu ya sakata la wizi wa Tsh 306 bilioni
katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Aliyewahi kuwa mkuu wa wilaya
mbalimbali nchini, Lapilali Ole Molloiment alisema kitendo cha Rais Kikwete
kuchelewa kutoa maamuzi, katika sakata la Escrow kumechangia sana kuondoa imani
ya wananchi kwa CCM.
"Kama Bunge letu, tayari
lilitoa mapendekezo, kwanini Rais amechelewa kutoa maamuzi, hili ni tatizo
ambalo limechangia CCM kushindwa,"alisema.
Alisema Watanzania wa sasa ni
tofauti na zamani, wanajua vitu vingi hivyo, ni vigumu kuwaficha mambo ambayo
yapo wazi na ambayo yanagusa maisha yao.
"Mimi ninachoona washauri wa
Rais ndio wanampotosha hili suala la Escrow, jambo hili lilitawala kampeni za
Ukawa, hivyo ilipaswa kulifanyia maamuzi mapema na kuzima maneno kuwa CCM
inawatetea waliohusika,"alisema.
"Mimi ni Kada wa CCM, nasema
tusipobadilika na kuwaondoa wachache wanaotuvuruga, tujiandae kuwa chama kikuu
cha upinzani mwaka 2015,"alisema.
Kada Mwingine wa CCM, Joram Kaaya
alisema, matokeo wa Uchaguzi wa Serikali za mtaa yana maana kubwa kwa uchaguzi
ujao hivyo, ni muhimu kwa CCM kujipanga.
"Lazima CCM tujipange
haiwezekani watu wachache wavuruge chama alafu tubaki, mimi naungana na Katibu
Mkuu wetu, Kinana wote waliohusika na haya mambo ya Escrow waondoke,” alisema
Kaaya.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment