Ni janga kwa sababu watu waishio mabondeni hupoteza maisha, hupoteza
makazi, hupoteza mali na hupoteza biashara zao, ingawa huwachukua muda
mfupi kurejea kwenye makazi hayo mara tu mvua zinapoisha.
Kwa kawaida mvua ni neema kutokana na faida
nyingi inazoleta kwa jamii, hasa kwa nchi maskini kama Tanzania ambazo
hutegemea sana kilimo ambacho hakijaendelezwa sana kiasi cha kuwa cha
kisasa kwa sehemu kubwa ya nchi.
Kwa maana hiyo, mvua ni baraka kwa kuwa ndio
tegemeo kubwa la mafanikio katika kilimo endapo wananchi wanaelekezwa
vyema kuhusu matumizi mazuri ya vipindi vya mvua. Faida nyingine ni kama
maji kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ingawa bado wananchi
hawajaeleweshwa wala kupewa stadi za kutosha za uvunaji maji.
Pia, kwa Jiji la Dar es salaam, ni sawa kabisa
wanaposema “watu wa Dar es Salaam wanaogopa mvua kuliko magari” kwa kuwa
mvua ni janga, hata iwe ya saa chache kama ilivyokuwa Jumatatu.
Ni janga kwa sababu watu waishio mabondeni
hupoteza maisha, hupoteza makazi, hupoteza mali na hupoteza biashara
zao, ingawa huwachukua muda mfupi kurejea kwenye makazi hayo mara tu
mvua zinapoisha.
Ni janga kwa sababu mvua zinaponyesha barabara
nyingi hazipitiki na hivyo kusababisha foleni kubwa kwenye barabara
zinazopitika kwa sababu magari yote hukwepa barabara mbovu na kutumia
chache nzuri.
Lakini ni janga kubwa kwa sababu miundombinu ya
majitaka, si tu ni mibovu, bali pia hailingani na mabadiliko makubwa
ambayo jiji limepitia katika miaka michache ya hivi karibuni; kushamiri
kwa majengo mengi katikati ya mji na majengo ambayo yanazuia mikondo ya
maji kuelekea baharini isifanye kazi vizuri.
Hili ni tatizo ambalo linaonekana kuwa la kawaida
sasa na si ajabu viongozi wetu wanaposikia mvua kubwa imenyesha,
hufahamu kuwa baadhi ya maeneo yamefurika maji kwa sababu, kwanza, njia
ambayo zingetumiwa na maji hayo kuelekea baharini zimebanwa kutokana na
ujenzi holela na pili, miundombini ya majitaka inazidiwa na wingi wa
maji yanayoongezewa na mvua.
Kwa hiyo, ni jambo ambalo linaonekana la kawaida
kuona vinyesi vikisambaa kwenye mitaa ya katikati ya jiji baada ya mvua
kidogo kunyesha, picha za magari yaliyokwama kwenye maji katikati ya mji
na picha za nyumba zinazoonekana paa tu mita chache kutoka katikati ya
jiji.
Haya huanikwa kila wakati mvua zinaponyesha na
hatujui wala hatuoni mkakati wowote mkubwa ukichukuliwa kuhakikisha
miundombinu ya majitaka inapanuliwa ili istahimili ongezeko la majengo
katikati ya jiji. Haiboreshwi kuhakikisha inadhibiti uwingi wa maji
yanayosababishwa na mvua zinazoweza kuwa kubwa kama ilivyokuwa juzi.
Hatujui kama viongozi wetu wanaguswa na matatizo
haya, ambayo ni kero kubwa hasa kwa wananchi wa kawaida au wameshayazoea
kwa kuwa hutokea kila mwaka na baada ya mvua kuisha husahauliwa?
Hivi hadi lini viongozi wetu wataendelea kuona
tatizo hili la mvua linahitaji mkakati mkubwa wa kukabiliana nalo? Hivi
ni lini viongozi wetu wataona kuwa miundombinu ya majitaka haistahimili
ongezeko la majengo linalosababisha ongezeko la majitaka? Hivi ni lini
wataona kuwa miundombinu ya majitaka haistahimili ongezeko la maji
yanayoletwa na mvua?
Hivi itakuwa ni nchi gani ambayo wananchi wake
wanaandaliwa kuzoea matatizo badala ya viongozi kushughulika kuwatatulia
kama wanavyoahidi wakati wakitoa jasho kuomba madaraka?
Sisi tunadhani kuwa wakati huu tunajiandaa kuingia mwaka mpya, viongozi wetu waanze kuyachukia matatizo na kufikiria njia za kuwapunguzia wananchi wao kero za kila mwaka ili waanze kuishi kwa matumaini.
CHANZO: MWANANCHI
Sisi tunadhani kuwa wakati huu tunajiandaa kuingia mwaka mpya, viongozi wetu waanze kuyachukia matatizo na kufikiria njia za kuwapunguzia wananchi wao kero za kila mwaka ili waanze kuishi kwa matumaini.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment