Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Ethiopia bado ni
nchi isiyoendelea, ni miongoni mwa nchi maskini duniani. Sasa umaskini
umepungua Ethiopia na uchumi unachangamka. Mwaka 2013 ulipanda kwa
asilimia kumi.
Hivi karibuni Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam
Desalegn, alitembelea Ujerumani kwa siku tatu na kufanya mazungumzo na
Kansela Angela Merkel pamoja na wafanyabiashara wa Kijerumani juu ya
ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Hadi ifikapo mwaka 2025, Ethiopia inataka kugeuka
kuwa nchi yenye wakaazi wenye vipato vya wastani. Kufikia lengo hilo
Serikali ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika inahitaji wawekezaji.
Hilo haliepukiki. Alipokuwa mjini Berlin,
Hailemariam aliwaambia waandishi wa habari kwamba tayari Waasia wako
nchini mwake, akimaanisha bila shaka, Wachina ambao wamewekeza kwa wingi
katika nchi hiyo.
Lakini sasa alisema, Waethiopia wanataka
wawekezaji wa kutoka nchi mbalimbali. Hayo ni maneno ya busara, kwani ni
hatari mtu kutia mayai yake yote katika kikapu kimoja. Kwa hivyo, China ambayo kwa miaka sasa imekuwa
ikiwekeza kwa kasi kubwa Barani Afrika haitakuwa mshirika wa kiuchumi
pekee huko Addis Ababa. Nao wafanyabiashara wa Kijerumani kutokana na tamko hilo la Hailemariam, hawajazubaa.
Kabla mkuu huyo wa Serikali kuondoka Berlin
wafanyabiashara wa Kijerumani walikuwa mbioni kufanya mazungumzo na
ujumbe kutoka Ethiopia uliofuatana na waziri mkuu huyo wakitafuta masoko
ya nini wanachoweza kuuza na kununua kutoka Ethiopia.
Usafirishaji
Naam. Katika biashara anayengojangoja, kama wanavyosema Waswahili, atakuta mtoto si wake.
Inatarajiwa kwamba Februari mwakani treni 41 mpya
kabisa zitakuwa zinatembea katika mji kuu wa Addis Ababa. Kwanza
zitaanza kwa majaribio na Mei zitakuwa tayari zinabeba abiria.
Licha ya Afrika Kusini hizo zitakuwa treni za
mwanzo za barabarani zinazosukumwa kwa nguvu ya umeme kuweko chini ya
Jangwa la Sahara. Hii ni habari nzuri, licha ya kwamba, kwa mujibu wa Umoja wa
Mataifa, Ethiopia bado ni nchi isiyoendelea, ni miongoni mwa nchi
maskini duniani.
Uzalishaji umeme
Hata hivyo, treni hizo za barabarani ni alama
tosha kwamba nchi hiyo iko katika njia sahihi ya maendeleo. Tusisahau
kwamba nchi hiyo ilikumbwa na balaa kubwa la njaa katika miaka ya
themanini iliyosababisha vifo vya maelfu kwa maelfu ya raia. Sasa umaskini umepungua Ethiopia na uchumi
unachangamka sana. Mwaka 2013 ulipanda kwa asilimia kumi na mwaka huu wa
2014 na miaka michache ijayo unatazamiwa utaimarika na kwenda juu kwa
asilimia saba.
Hizo ni tarakimu nzuri ukilinganisha na zile za
nchi zinazoizunguka Ethiopia. Na kumbuka Ethiopia haina ule utajiri wa
mali asili za ardhini kama vile Nigeria au Afrika Kusini.
Uchumi wa nchi hiyo umepanda kwa vile Serikali
nayo inawekeza, na mapato ya nchi hiyo yameongezeka kutokana na kahawa
yake nzuri inayouzwa ng’ambo. Kwa hivyo, Serikali ya nchi hiyo inaponadi kwamba
ifikapo mwaka 2025 nchi hiyo itakuwa na wakaazi wenye vipato vya kati na
kati, hiyo si porojo tu. Inawezekana. Waziri Mkuu, Hailemariam si mwanasiasa mwenye
kupayuka sana. Huzungumza polepole na hajinati. Hatumii neno Mimi“, bali
mara nyingi huanza tamko lake kwa kusema‚ Sisi au Serikali ya Ethiopia.
Kinyume na alivyokuwa mtangulizi wake, Meles
Zenawi, aliyeingia madarakani akiwa ana umri wa miaka 36 na kuaga dunia
mwaka 2012, aliwekeza juhudi katika uchumi. Naye alifanikiwa katika hilo. Uchumi wa Ethiopia umekuwa ukipanda mfululizo tangu kuondoka utawala wa kikoministi wa Mengistu.
Serikali yake iliweka uzito katika kuboresha miundombinu iliyokuwa mibovu sana hapo kabla na kukifanya kilimo kiwe cha kisasa.
Uzalishaji umeme
Mradi mkubwa wa Bwawa Kubwa la Mapambazuko ya
Ethiopia linalojengwa katika Mto Nile na ambalo mwaka 2017 litaweza
kutoa umeme wa nguvu za Megawatt 6000, utatanzua matataizo ya nishati
katika nchi hiyo. Meles Zenawi aliitawala nchi kama vile wanavyofanya wanajeshi
mara nyingi, kimabavu. Lakini kutokana na mafanikio ya kiuchumi, Chama
Tawala cha EPRDF kinaungwa mkono na wananchi wengi.
CHANZO: MWANANCHI
Lakini wapinzani wa Serikali wanaripoti juu ya
maofisa wa usalama kupeleleza sana nyendo za raia na kwamba uhuru wa
watu kutoa maoni yao unawekewa pingamizi.
Mwaka 2005, Zinawi alitumia mabavu, kupitia majeshi ya usalama, kuzuia maandamano ya upinzani.
Katika Ethiopia, nchi yenye makabila makubwa
mbalimbali, kuna makundi yenye kutaka maeneo yao yawe na mamlaka makubwa
zaidi ya utawala, na pia kuna makundi mengine yenye kutaka maeneo yao
yajitenge kabisa. Kuna makundi ya waasi yaliyotangazwa na Serikali
kuwa ni ya kigaidi na watu wanaoyaunga mkono au kushukiwa kuyaunga mkono
huandamwa na kusumbuliwa.
Alipokuwako Berlin, Hailemariam aliyakanusha
malalamiko yaliyotolewa na Shirika la Kupigania Haki za Binadamu Duniani
(Amnesty International) ambalo lilidai kwamba watu wa Kabila la Waoromo
wanakandamizwa nchini Ethiopia. Alisema madai hayo ni ya uongo na kwamba Waoromo wanaridhika na Serikali ila alisema kila aliye gaidi ni mhalifu. Lakini njia anayofuata Hailemariam, licha ya yeye
mwenyewe kukanusha, ni kinyume na ile alioifuata Meles Zenawi. Yeye
anadai njia ni ileile ila wao ni watu wawili tofauti.
Ethiopia, nchi yenye wakaazi milioni 90 hivi sasa,
licha ya kukosa demokrasia iliyo pana, inaashiria itakuwa na uchumi
mkubwa katika miaka ijayo. Imefaidika kuwa na uzito wa kisiasa, kiuchumi na
kijeshi hivi sasa kwa vile watawala wake wamekuwa washirika wakubwa
katika vita vya kupambana na ugaidi katika eneo la Pembe ya Afrika.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment