Rais
wa Tanzania Jakaya Kikwete leo atalihutubia taifa la nchi hiyo ambapo
anatarajiwa kuyatolea ufafanuzi masuala nyeti yanayoligusa taifa hilo.
Wadadisi
wa masuala ya kisiasa na kijamii wanatabiri huenda hatua
atakazozichukua dhidi mawaziri na maafisa wa serikali waliohusika na
ufisadi wa mamilioni ya fedha katika akaunti ya Escrow itakuwa ni moja
kati ya agenda muhimu atakayoitolea ufafanuzi.
Hotuba hiyo inakuja
wakati kukiwa na shinikizo kutoka kwa baadhi ya raia na wapinzani
wakitaka hatua zaidi zichukuliwe kutekeleza azimio la bunge ambalo
linatataka mawaziri na maafisa wa serikali waliohusika na sakata hilo la
ufisadi wawajibishwe ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi.
Sakata la Akaunti ya Escrow
liliibuliwa bungeni na mmoja wa wabunge wa bunge la Tanzania, David
Kafulila na kusababisha mjadala mkali na kuamua Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Hesabu za Serikali kupewa jukumu la kuchunguza kashfa hiyo. Baada
ya uchunguzi kuwasilishwa katika mkutano wa bunge uliomalizika mwishoni
mwa mwezi Novemba, kamati hiyo ilikuja na maazimio manane kuhusu
taarifa ya ukaguzi maalum kuhusiana na miamala iliyofanyika katika
akaunti ya Escrow ya Tegeta pamoja na umiliki wa kampuni ya IPTL.
Miongoni
mwa maazimio ya bunge yaliwataja baadhi ya wanasiasa, mwanasheria mkuu,
maafisa waandamizi wa serikali, majaji, wakuu wa taasisi za umma,
viongozi wa dini, mawakili wa kujitegemea na watu binafsi kuhusika
katika kashfa hii na hivyo kuagiza mamlaka zinazohusika kuwachukulia
hatua za kisheria wahusika na wengine kuondolewa katika nyadhifa zao za
kuteuliwa,tayari Mwanasheria mkuu wa serikali amekwisha jiuzulu na rais
kukubali uamuzi huo.
Akaunti ya Escrow ilianzishwa katika Benki
Kuu ya Tanzania ili kuhifadhi fedha, baada ya kuibuka kwa mvutano kati
ya Shirika la Umeme la Tanzania, Tanesco na kampuni ya kufua umeme ya
IPTL kuhusu ongezeko la mtaji wa uwekezaji, huku TANESCO ikilalamika
kuwa gharama za kununua umeme kutoka kampuni ya IPTL zilikuwa za juu
mno. Fedha hizo zingeendelea kutunzwa katika Akaunti hayo hadi wakati
ambapo suluhisho la mvutano wa wabia hao wawili lingepatikana.
CHANZO: BBC SWAHILI
No comments:
Post a Comment