Pages

Thursday, December 11, 2014

DK. SLAA APINGA RIPOTI YA CAG KUHUSU ESCROW KUTANGAZWA

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amesema agizo hilo la Rais Jakaya Kikwete la kuweka ripoti ya ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika akaunti ya Tegeta Escrow kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ili wananchi waisome halina jipya bali linalenga kuchelewesha kuwachukulia hatua wahusika.
Juzi Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ilitoa taarifa ikisema kuwa Rais Kikwete atafanya maamuzi kuhusu maazimio ya Bunge kuhusu vigogo waliohusishwa na sakata la Escrow kuanzia wiki ijayo na kuwa  ameagiza ripoti hiyo itangazwe ili wananchi wengi waisome kabla ya maamuzi hayo.
Dk. Slaa alisema jambo ambalo Watanzania wanatarajia kutoka kwa  Rais hivi sasa ni kuwachukulia hatua wahusika na siyo kuagiza hayo anayosema ambayo lengo lake ni kuwasahaulisha Watanzania. Alisema kama Rais alikuwa  na lengo la kufanya hivyo angefanya mapema, lakini kwa sasa hivi kinachotakiwa ni utekelezaji.
Dk. Slaa aliongeza kuwa kama ni uchunguzi tayari umekwisha fanywa na kukamilishwa na vyombo husika.
“Rais ana Usalama wa Taifa, mashushushu, Interpol, alishindwa kufanya hivyo mapema?” alihoji na kuongeza: “Anatuambia hivyo sasa wakati Watanzania wanachosubiri ni kusikia yeye amechua hatua, hana jipya.”
“Ameona wahusika wote ni vigogo kwa hiyo anataka kuzimazima,” alisema.
Bunge lilimshauri Rais awawajibishe Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo; Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment