Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi
(katikati), akipokea tuzo kutoka kwa Mwenyekiti wa Tanzania Saccos for
Women Entrepreneurs (Taswe), Anna Matinde (kulia), wakati wa uzinduzi
rasmi wa Saccos hiyo, jijini Dar es Salaam juzi. Kushoto ni Naibu Balozi
wa India nchini, Balvinder Humpal.Tuzo hiyo ni kutambua mchango wa Dk.
Mengi katika kusaidia jamii.
Ushauri huo ulitolewa na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, wakati akizindua Chama cha Kuweka na Kukopa cha Taswe Saccos, juzi jijini Dar es Salaam.
Dk. Mengi, ambaye katika uzinduzi huo aliambatana na Naibu Balozi wa India nchini, Balvinder Humpal, aliwataka wajasiriamali wanaounda chama hicho kuwa waaminifu wa kurejesha mikopo ili biashara zao zisifie njiani. “Uhai wa Saccos ni pale wanachama wake wanapokuwa waaminifu katika kukopa na kurudisha, kama hawarudishi madeni, Saccos itakufa,” alisema Dk. Mengi. Alitaja baadhi ya mambo, ambayo wanachama wa Saccos wanapaswa kuyazingatia ili chama chao kiendelee kuwa ni pamoja na kujiamini na kuwa na macho yanayoona fursa.
Mengine ni kuwa waaminifu katika kurudisha mikopo, kuhakikisha ubora wa vitu au bidhaa wanazozitoa, kuwa na vifaa vya teknolojia ya kisasa, kama vile kompyuta ili kuitangaza biashara yao ndani na nje ya nchi.
Pia aliwataka kuwa na elimu ya kutosha kuhusu utunzaji wa hesabu kwa ajili ya kukifanya chama chao kupiga hatua nao kukabiliana na hali ya umaskini.
Vilevile, aliwataka kuwa wabunifu kwa kuliona tatizo kuwa ni fursa, kwani uwezo wa kufanya hivyo wanao.
Pia alitunukiwa tuzo na wanachama hao kwa kutambua mchango katika kusaidia jamii. Aliahidi kukichangia chama hicho Sh. milioni 50, ambacho hadi wakati wa uzinduzi kilikuwa na mtaji wa Sh. milioni 50.
Mwenyekiti wa Saccos hiyo, Anna Matinde, aliema chama hicho ni taasisi ya kifedha iliyoanzishwa kwa ajili ya kuwawezesha Watanzania kuweka akiba, kununua hisa na kupata mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya shughuli zao za kibiashara na kukabiliana na wimbi la umaskini.
Alisema Saccos hiyo ina miradi mbalimbali, ikiwamo ya majiko ya kisasa kwa ajili ya kuwawezesha wanachama wake, ambao kwa sasa wanafikia 150.
Matinde alisema malengo ya baadaye ya chama hicho ni kufungua matawi mengine nchini na kwamba, hadi Machi mwakani, wanatarajia kufungua matawi katika baadhi ya mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Pwani, Dodoma na Mtwara.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment