Dodoma/Dar/Mikoani. Ni wiki ya
shida. Wiki hii inatarajiwa kuwa ya vikao mfululizo na mijadala
isiyokoma. Ndiyo wiki inayotarajiwa kuuweka hadharani mtikisiko wa tano
katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete wakati ripoti ya uchunguzi wa
sakata la IPTL itakapowasilishwa rasmi kwa wabunge na Taifa kwa jumla
mjini Dodoma keshokutwa na kuhitimisha minong’ono na uvumi.
Ni wiki ambayo Bunge litaamua juu ya hatua za
kuchukua dhidi ya vigogo wa Serikali ambao wamekuwa wakitajwa kuhusika
na ufisadi huo wa kuchota au kunufaika na Sh306 bilioni katika Akaunti
ya Tegeta Escrow iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Ripoti hiyo inayosubiriwa, itawasilishwa na Kamati
ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), inayoongozwa na Zitto Kabwe,
ambayo itatoa mapendekezo juu ya hatua za kuchukua.
Wabunge wa vyama mbalimbali, jana walikuwa na
vikao kadhaa wakijipanga jinsi ya kushughulikia sakata hilo mara tu
ripoti itakapowasilishwa.
Wabunge wa CCM jana jioni walikutana kuwekeana
msimamo kuhusu sakata hilo huku kukiwa na taarifa kwamba baadhi yao,
hasa walioonyesha kushabikia ripoti hiyo, wamekaripiwa na kupewa
mwongozo wa kuilinda Serikali. Habari za ndani zinasema kuna juhudi kubwa
zinafanywa ili kuhakikisha Baraza la Mawaziri halivunjwi kwa mara ya
pili, baada ya tukio la mwaka 2007 alipojiuzulu aliyekuwa Waziri Mkuu,
Edward Lowassa kutokana na kashfa ya Richmond.
Habari zaidi zilisema, juzi kilifanyika kikao
kingine ndani ya Makao Makuu ya CCM, Dodoma kikiwahusisha baadhi ya
wabunge, mawaziri na vigogo wanaotuhumiwa katika kashfa hiyo.
Habari zinasema kikao hicho kilipata muhtasari
kutoka ndani ya PAC lakini hakikufikia mwafaka kutokana na baadhi ya
wajumbe kupinga kujadili suala hilo mbele ya watuhumiwa na bila kupewa
ripoti kamili ya Mdhibiti na Mkaguzi na Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG).
Vilevile, wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani
wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) nao walikutana jana
kujipanga kwa ajili ya kushughulikia sakata hilo.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alisema wameitisha kikao hicho kuwekeana msimamo.
“Tunakwenda kukutana kama Ukawa ili tuwekeane
msimamo jinsi gani ya kulishughulikia sakata la ufisadi wa Escrow,”
alisema Mnyika.
Ripoti hiyo itawasilishwa huku kukiwa na madai
kutoka Ukawa kuwa imevuja na kusambazwa mitaani na baadhi ya kurasa
zenye majina ya wahusika zikichomolewa ili kuuhadaa umma.
Lipumba amvaa Pinda
Kurasa zilizochomolewa zimeelezwa kutawanywa kwa wabunge na mtu
mmoja ambaye Ukawa haujamtaja, lakini ukitaka polisi imshughulikie.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime
juzi alithibitisha kumshikilia mhusika baada ya kumkamata akiwa na
nyaraka za Bunge ambazo hazipaswi kuwa mikononi mwake.
Alisema walipokea taarifa za mtu huyo kutoka Ofisi
ya Bunge na walipomkamata na kumpekua walikuta nyaraka za aina tatu,
mbili zikiwa na muhuri wa Katibu wa Bunge na alipohojiwa alisema amepewa
na mbunge mmoja aliyeambatana na watu wengine wawili (hakuwataja) ambao
bado wanatafutwa.
Lipumba amvaa Pinda
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
amemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kujiuzulu au kufukuzwa kwa kushindwa
kuzuia ufisadi wa fedha katika akaunti hiyo. Pia amemtaka Pinda
awajibike kwa kauli yake kwamba fedha hizo hazikuwa za umma.
Lipumba aliwataja vigogo wengine wanaotakiwa
kujiuzulu kuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema,
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu
wake, Eliakimu Maswi.
Kadhalika, Profesa Lipumba amevitaka vyombo vya
dola kuwakamata na kuwafungulia mashtaka haraka iwezekanavyo wamiliki wa
Kampuni ya IPTL, James Rugemalira na Habinder Singh Sethi kutokana na
kashfa hiyo. Rugemalira na Seth wanadaiwa kuchukua Sh321
bilioni kinyume na makubaliano kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow ambayo
ilifunguliwa baada ya kutokea mgogoro wa malipo kati ya Tanesco na IPTL. Fedha hizo zilichukuliwa kabla mgogoro huo haujapatiwa suluhisho, kitendo kinachotafsiriwa kuwa kilikuwa na mazingira ya rushwa.
Profesa Lipumba alisema akaunti ambazo vigogo wa
Serikali walipitishia fedha kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow
zinatakiwa kusimamishwa.
Maaskofu wambana Pinda
Maandamano CUF
Lipumba alisema chama hicho kwa kushirikiana na
wadau wengine wanaandaa maandamano kulaani vitendo vya kifisadi kwenye
Akaunti ya Tegeta Escrow na kuwapongeza wabunge walioibua hoja hiyo hadi
ukaguzi ukafanywa na CAG.
Alisema maandamano hayo yatafanyika baada ya mjadala wa siku mbili utakaofanyika bungeni kuhusu sakata hilo. Alisema baada ya wabunge kujadili watafanya maandamano hayo ili kufikisha ujumbe kwa wananchi kuhusiana na ufisadi huo.
Maaskofu wambana Pinda
Kwa upande mwingine, Serikali imetakiwa kutoa
majibu ya msingi juu ya sakata la IPTL ili kuepusha minong’ono inayoweza
kusababisha uvunjifu wa amani nchini.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk
Jakob Chimeledya alisema jana kuwa suala la escrow limeiweka Serikali
katika hali mbaya kiasi kwamba inaweza isiaminike kwa wananchi wake.
Hata hivyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda hakujibu
hoja hiyo moja kwa moja badala yake akasema inapokaribia kipindi cha
uchaguzi kunakuwa na mambo mengi ambayo hujitokeza.
“Mara nyingi inapokaribia kipindi kama hiki si
mnajua mbio zilizoko mbele yetu? Kwa hiyo kuna mambo yanakuwa ya kweli
na mengine siyo ya kweli, inabidi tuangalie, lakini Serikali itaona
namna ya kutoa maelezo,” alisema Pinda.
Akizungumza mbele ya mamia ya waumini wa Kanisa
hilo katika ibada ya kumweka wakfu Askofu wa sita wa Dayosisi Central
Tanganyika (DCT), Dk Dickson Chilongani, Askofu Chimeledya alisema
ukimya wa Serikali unatia shaka.
“Tunaitaka Serikali itoe ukweli kwani sasa Taifa
linaishi kwa uvumi tu jambo ambalo si la kufumbia macho na kama hivi
ndivyo hamtaaminika,” alisema Askofu Chimeledya.
Mbeya na Arusha
CHANZO: MWANANCHI
Mwandosya: Hatutaangalia mtu
Wakati huo huo; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi
Maalumu), Profesa Marc Mwandosya amesema mbivu au mbichi kuhusu sakata
hilo zitajulikana wiki hii na hataangaliwa mtu, bali masilahi ya chama.
Profesa Mwandosya alisema hayo jana wakati
akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ambao ni wafuasi wa
CCM waliopata nafasi ya kumhoji masuala mbalimbali ya chama na Serikali.
Alisema angependa watu wanaotajwa wajiondoe
wenyewe hata kama hawajahusika, kwa kuwa itakuwa ni nzuri kwao na
itakuwa heshima kwa chama... “Hata kama mtu hajahusika itamsaidia sana
akijiondoa kwani italinda chama pia.”
Alisema kwa kuwa suala hilo linajadiliwa ndani ya
vikao vya chama ambavyo naye huwa anaingia, atatoa ushauri na kuangalia
jinsi gani ya kulishughulikia.
Mbeya na Arusha
Mwenyekiti Mstaafu na Mwasisi wa CCM mkoani Mbeya,
Isakwisa Mwambulukutu ameshauri watu wote watakaobainika warudishe
fedha na kufilisiwa mali zao na kama ni viongozi wa umma, waachishwe
nyadhifa zao zote na wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua
Nassari amewataka wakazi wa jimbo lake kutochangia ujenzi wa maabara
hadi watuhumiwa waliohusika na fedha za escrow watakapowajibishwa na
kuzirejesha “... huu ndiyo ujumbe wangu leo hapa Kanisani.”
Alisema hayo katika ibada ya kusimikwa wachungaji
Barakaeli Mungure na Lazaro Mafie wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT), Usharika wa Mulala.
Nape
Kutoka Lindi, viongozi wa juu wa CCM wamesema kila
mtu atabeba msalaba wake mwenyewe katika sakata hilo kwa kuwa chama
hicho hakiwezi kuwavumilia viongozi na watendaji wenye nia mbaya na
Serikali yake. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
alisema katika mkutano wa hadhara mjini Lindi jana kuwa, chama hicho
ndicho mwasisi wa maadili na miiko ya uongozi wa umma nchini kuanzia
enzi za Tanu, hivyo kitaendelea kusimamia kwa vitendo dhana hiyo.
Alisema kinyume na wapinzani wanavyodai kuwa CCM
imeondoa kipengele cha maadili ya umma kwenye Katiba Inayopendekezwa,
chama hicho kitaendelea kuyasimamia bila woga maadili kama kilivyochukua
uamuzi mgumu katika matukio ya Richmond na mengine.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema
wakati wa kuomba ridhaa kwa wananchi waliahidi mambo mengi, hivyo ni
wajibu wa chama kurudi kuangalia utekelezaji wake.
Alisema muda wa kuvumiliana, kubebana na kulindana
umekwisha kwani imekuwa tabia na ugonjwa kwa baadhi ya viongozi
kushindwa kusimamia na kukosoa pale watendaji wanaposhindwa kuwajibika
ipasavyo na CCM haiwezi kufumbia macho mwenendo huo.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment