Pages

Monday, November 24, 2014

WASOMI WATAKIWA KUISAIDIA TANZANIA KUKUZA UCHUMI

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi amewataka wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya juu vya mkoani hapa watumie fursa waliyonayo kuisaidia Tanzania isonge mbele na kufikia uchumi wa juu zaidi.
Alitoa nasaha hizo mwishoni mwa wiki iliyopita  wakati akizungumza na wanavyuo hao kwenye ukumbi wa Chimwaga, Dodoma wakati wa mkesha wa kusifu na kuabudu (Dodoma Campus Night) ulioandaliwa maalum kwa ajili ya kuwajenga kimaadili wanafunzi wa vyuo vya mkoa huo.
Dk. Nchimbi ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kabla ya kuhamishiwa Njombe, aliwaasa wanafunzi hao waache kuendekeza matumizi ya simu za mkononi kwa kutumiana meseji ambazo zinawatoa kwenye umakini wa masomo yao.
“Inasikitisha kuona mwanafunzi akiingia mwaka wa kwanza anakuwa mwema, lakini baada ya muda anarudi nyuma kimaendeleo… kisa meseji anazotumiwa”.
“Muwe makini na masomo yenu. Angalieni mavazi yenu, angalieni mienendo yenu, jichungeni msiyumbishwe na tabia za makundi lakini kikubwa zaidi ni kutambua nafasi mlizonazo na kusimama imara ili kuisadia nchi hii isonge mbele na kufikia uchumi wa juu zaidi,” alisema.
Mapema, akimkaribisha kuzungumza na wanafunzi hao, Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la TAG-ICC Dodoma, Dk. Gerald Ole Nguyaine aliwaambia wanavyuo kwamba wanapaswa kuiheshimu nafasi hiyo ya pekee ambayo Mungu amewapa.
Naye Mchungaji Casey Kalaso wa Kanisa la Utume wa Kristo kutoka Kabwe nchini Zambia,  aliwataka wanavyuo hao watambue kuwa mafanikio yanakuja pale mtu anapofanya maandalizi na kutumia vizuri fursa aliyonayo.
“Changamoto kuwa inayotukabili hivi sasa ni kwa mwanadamu kutojua majira aliyomo… Watu wengi hatujui nini tunapaswa kufanya na kwa wakati gani. Usipokuwa mwangalifu utalia baadaye wakati ulichezea fursa uliyoipata sasa,” alisema.
Akitumia mfano wa Samson na Delila kutoka kitabu cha Waamuzi (sura ya 13), aliwataka waithamini nafasi waliyonayo kwani ikipotea ni nadra kuipata tena na kuitumia vizuri. “Usiangalie mambo ya nyuma, angalia nafasi ya sasa unayopewa na Mungu na uifanyie kazi. Jihadhari na watu wanaokuja maishani mwako, wako wanaokuja kukuongezea thamani lakini wengine wanakuja ili kukufanya uwe dhaifu zaidi,” aliwaonya.
 Mchungaji Mathew Sasali wa Kanisa la TAG Mbeya, aliwataka wanavyuo hao wajitambue nafsi zao na kubaini ni picha gani ambazo zimechorwa maishani mwao kama kweli wanataka kusonga mbele maishani mwao.
“Kuna watu waliambiwa hutafaulu kwa sababu katika ukoo wenu hakuna msomi, au fulani hutaolewa kwa sababu katika familia yenu hakuna aliyewahi kuolewa. Hizo zote ni picha zinazochorwa kwenye maisha ya watu na kuwazuia kufikia malengo wanayotamani kuyapata maishani mwao,” alisema.
Alisema njia pekee ni kuibadilisha na kupambana na picha iliyowekwa mbele ya maisha yao.  “Picha iliyo mbele yako siyo ile ambayo Mungu ameileta mbele yako. Taifa la Israel lisingeweza kwenda mbele kama picha nyingine isingechorwa mbele yao ambayo ilibadilishwa na Yoshua na Kaleb,” alisisitiza.
Katika mkesha huo uliohudhuriwa na wanavyuo zaidi ya 5,000, yalifanyika pia maombi kwa ajili ya vijana wote wa Tanzania, uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Uchaguzi Mkuu wa 2015 na  Katiba Inayopendekezwa.
Wanavyuo hao wa dini mbalimbali wanatoka vyuo vikuu vya Dodoma (UDOM), St. John’s, Vyuo vya Mipango, Madini, Mirembe, Hombolo, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na vyuo vya ualimu vya Mitumba na Capital.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment