Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira amesema ubora wa mgombea
ndiyo utakaokuwa msingi wa ushindi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Desemba 14 na Uchaguzi Mkuu 2015.
Akizungumza mjini Arusha mwishoni mwa wiki, Wasira
anayetajwa kuwa mmoja wa watu wanaowania kuteuliwa kugombea urais
kupitia CCM, alisema hakuna chama kitakachoshinda kwa kutegemea umaarufu
wake au wingi wa wanachama wake.
Alisema upigaji kura ungekuwa unazingatia chama,
basi CCM isingehangaika kupiga kampeni na kujinadi kwani ndicho chenye
wanachama wengi nchini na hivyo kingeshinda kirahisi.
Utafiti wa Twaweza
Akijibu swali la nini maoni yake kuhusu utafiti wa
Taasisi ya Twaweza kuhusu urais mwakani, Wasira alisema: “Kwanza
sijausoma utafiti wenyewe kujua vigezo na sampuli ya utafiti wao, lakini
lililodhahiri ni kwamba ubora wa mgombea au wagombea ndiyo msingi wa
ushindi kwenye uchaguzi.”
Waziri huyo aliyekuwa jijini Arusha kuhudhuria
vikao vya CCM kupitia nafasi yake ya ulezi wa chama hicho Mkoa wa Arusha
alisema kipindi cha viongozi kufikiria ukubwa na umaarufu wa vyama vyao
nyakati za kampeni na uchaguzi kimepitwa na wakati, badala yake kila
chama lazima kiwapime, kuwachuja na kupata wagombea bora.
“Ndani ya CCM tayari tumebaini hilo ndiyo maana
tuko makini kwenye uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali kuanzia
chaguzi za ndani na nje ya chama,” alisema.
Alisema CCM na viongozi wake wanaujua ukweli huo
kuwa wananchi hawaangalii itikadi zao za vyama wakati wa kupiga kura,
bali ubora wa mgombea. “Wananchi hawapigi kura kwa kuzingatia uanachama
wa vyama vyao. Hapana! Wanaangalia ubora wa mgombea. Mgombea bora
hushinda hata kama chama chake kina wanachama wachache katika eneo
husika,” alisema na kuongeza:
“Nawatoa hofu wanaCCM kuhusu uchaguzi wa Serikali
za Mitaa na Uchaguzi Ukuu mwakani. Chama kitasimamisha wagombea bora ili
kujihakikishia ushindi kama uchaguzi uliopita.”
Azungumzia Ukawa
Akijibu swali la iwapo CCM imeingiwa hofu ya
kushindwa kwenye chaguzi kuanzia Serikali za Mitaa baada ya vyama vikuu
vya upinzani nchini vya kuungana na kuunda Ukawa, Wasira alijibu kwa
kejeli akisema:
“Hakuna anayekatazwa kuota ndoto. Kuota ndoto ni
jambo la kawaida na kila mtu anaruhusiwa kuota. Ila ukweli unabaki kuwa
ndoto ni ndoto tu, ndiyo maana anayeota akiamka hutambua kuwa alikuwa
ndotoni.”
Mnyukano CCM
Alisema Ukawa inayoundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF na
Chadema kufikiria ushindi dhidi ya CCM kwa kuungana kwao ni ndoto
itakayoyeyuka wakiamka usingizini.
Alisema ingawa muungano huo ni jambo jema kwa
vyama vya ushindani, lakini hauwezi kuwa tishio kwa CCM yenye misingi
imara, mtandao mpana na rasilimali watu kila pembe ya nchi kulinganisha
na vyama vingine vya siasa. “Licha ya changamoto na mabadiliko makubwa
katika uwanja wa siasa yanayotokea nchini, CCM bado kinaendelea kubakia
kuwa chama kikuu, imara na chenye misingi inayoihakikishia ushindi siyo
tu kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu, bali hata Uchaguzi
Mkuu ujao 2015,” anasema Wasira.
Mnyukano CCM
Akizungumzia minyukano ya wenyewe kwa wenyewe
ndani ya CCM kuwania nafasi ya kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama
hicho, Wasira alisema ni dalili ya kuimarika na kukubalika kwa chama
miongoni mwa wanachama wenyewe na jamii kwa ujumla.
“Chama kisichotoa matumaini hakiwezi kushuhudia
mnyukano wa wanachama kuwania uteuzi. Watu kuchuana na kushindana kwa
nguvu ndani ya chama ni kudhihirisha kuwa chama kiko hai na imara. Watu
hawawezi kugombania kisichofaa.
“Ukiona watu wanachuana kuwania uteuzi ndani ya
CCM ujue kinakubalika ndiyo maana watu wana matumaini ya kushinda
kufanikiwa malengo yao kupitia tiketi ya chama. Ingawa ubora wa mgombea
ni jambo la kuzingatiwa.”
Akizungumzia tuhuma za rushwa na rafu ndani ya CCM
Wasira alisema: “Kwamba kuna rushwa na matumizi ya
fedha kuwania uteuzi ndani ya CCM ni jambo ambalo siwezi kulizungumzia
kwa sababu sijalishuhudia. Lililo dhahiri ni kwamba wanaoshindwa au
waliowaunga mkono kushindwa lazima watalalamika.”
Hata hivyo, alisema CCM imeweka misingi na
utaratibu bora wa kudhibiti vitendo vya rushwa ndani na nje ya chama
kuhakikisha kinapata wagombea bora watakaokihakikishia ushindi dhidi ya
wagombea kutoka vyama vingine vya siasa.
“Wana CCM wasihofu. Chama kiko macho dhidi ya
vitendo vyovyote vinavyokiuka taratibu, kanuni na katiba ya chama. Kuna
vyombo na vikao vinavyofuatilia kila kinachoendelea kuanzia ngazi ya
mashina hadi Taifa na uteuzi wa wagombea utazingatia ubora mgombea
mwenyewe utakaotuhakikishia ushindi.”
Alisema vikao vya chama hicho kila ngazi
vitatumika kupitia na kufanya uteuzi kulingana na majukumu na madaraka
ya kikatiba na kuwataka wanachama kuacha malalamiko na hoja inayoweza
kusababisha nyufa ndani ya chama, hivyo kunufaisha vyama vingine.
Wasira alikuwa akirejea malalamiko ya baadhi ya
wanachama kuhusu kura za maoni ndani ya chama hicho kuwania uteuzi
kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa Desemba 14, mwaka huu na kwa nafasi
yake ya mlezi wa mkoa, alipokea malalamiko kutoka wilaya mbalimbali
kuhusu rafu zinazodaiwa kuchezwa ngazi ya vitongoji na vijiji.
CCM Mkoa wa Arusha ina historia ya kupoteza uchaguzi kutokana na
mgawanyiko unaosababishwa na matokeo au mchakato wa kura za maoni.
Mwaka 1995, Jimbo la Karatu lilinyakuliwa na Chadema kupitia Dk
Willibrod Slaa baada ya vikao vya uteuzi kupuuza maoni ya wananchi
kupitia kura za maoni kwa kumteua Patrick Quorro badala Dk Slaa
aliyeshinda kura za maoni.
Baada ya kukatwa jina, wananchi Karatu wakamwomba
Dk Slaa kuhamia Chadema na kugombea ubunge na alimbwaga Quorro
aliyesimamishwa na CCM.
CCM pia kilikipoteza kiti cha Arusha Mjini mwaka
2010 baada ya Chadema kupitia kwa mgombea wake, Godbless Lema kutumia
mpasuko uliosababishwa na kura za maoni ndani ya CCM.
Katika uchaguzi mdogo Arumeru Mashariki, Chadema
kiliishinda tena CCM kwa Joshua Nassari kuibuka kidedea dhidi ya Sioyi
Sumari ambaye uteuzi wake uligubikwa na tuhuma za matumizi ya fedha huku
ukiacha mpasuko ndani ya chama hicho tawala.
Kama alivyosema Wasira, matokeo ya majimbo hayo
matatu kunyakuliwa na Chadema dhidi ya wagombea wa CCM kunadhihirisha
kuwa wapigakura hawafuati vyama, bali ubora na ushawishi wa mgombea.
Kauli ya Wasira kuhusu ubora wa mgombea katika
ushindi inakuja siku chache baada ya taarifa ya utafiti wa Twaweza
kuonyesha kuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na aliyempokea
nafasi hiyo, Mizengo Pinda, wote kutoka CCM wanaongoza kwa kuungwa na
mkono na wengi katika ngazi ya urais. Hata hivyo, wanasiasa, wasomi na
makundi mbalimbali ya kijamii wamepinga utafiti huo wakidai umeacha
maswali mengi likiwamo la kwa nini haukushirikisha wanawake ambao nao
wanatajwa urais 2015?
Wanaopinga utafiti huo pia wanatoa hoja kuwa wengi
wa waliohojiwa wana wastani wa miaka 50 na kuendelea, kada
inayosadikika kukiunga mkono CCM kulinganisha na vijana ambao wengi
wanaviunga mkono vyama vingine vya upinzani.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment