
Kivuko kilichopewa jina la MV Dar es Salaam, kimeletwa nchini jana
kutoka Bangladesh kikiwa cha kwanza kwa mwendokasi kuliko vingine vyote
nchini. Kina uwezo wa kubeba watu 300 waliokaa pamoja na
mizigo.
Wakazi wa Jiji
la Dar es Salaam sasa wataanza kusafiri kwa kutumia kivuko cha kisasa
kutoka katikati ya jiji hadi Bagamoyo na mikoa mingine badala ya kutumia
usafiri wa barabara.
Kivuko hicho kilichopewa jina la MV Dar es Salaam,
kimeletwa nchini jana kutoka Bangladesh kikiwa cha kwanza kwa
mwendokasi kuliko vingine vyote nchini. Kina uwezo wa kubeba watu 300
waliokaa pamoja na mizigo.
Akizungumza katika hafla ya kupokea kivuko hicho
kwenye Bandari ya Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuri
alisema ujio wa kivuko hicho chenye thamani ya Sh7.9 bilioni ni mwanzo
wa utatuzi wa kero ya foleni katika jiji hili.
Dk magufuli alisema kumekuwa na utegemezi mkubwa
wa usafirishaji kwa njia ya barabara, jambo ambalo linasababisha foleni
bila sababu ya msingi.
“Asilimia 99 ya mizigo husafirishwa kwa njia ya
barabara, wakati asilimia moja tu ikisafirishwa kwa ndege, treni na
meli. Hakuna haja ya kusafirisha makontena kwa njia ya barabara,
tunahitaji usafiri wa treni kusafirisha makontena kutoka bandarini
kwenda nje ya mji ili malori yakapakie huko,” alisema.
Alisema kwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza
adha ya foleni, ambayo mara nyingi husababishwa na malori yanayobeba
mizigo kutoka au kwenda bandarini, hasa katika Barabara za Mandela na
Kilwa.
Waziri huyo alibainisha miradi mingine ya
kupunguza foleni itakayotekelezwa jijini ni ujenzi wa barabara za juu
katika makutano ya barabara eneo la Ubungo na Tazara. Pia, ujenzi wa
Daraja la Kigamboni litakalokamilika Juni, mwakani na kugharimu Sh214
bilioni.
Alisema mradi mwingine wa Mabasi Yaendayo Kasi
(BRT) utagharimu Sh288 bilioni na unatarajiwa kukamilika Machi, mwakani.
Alibainisha kuwa bado ujenzi wa barabara za mzunguko unaendelea na
kumtaka mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kudhibiti wafanyabiashara
ndogondogo wanaoingilia hifadhi ya barabara na kusababisha foleni.
“Dar es Salaam inahitaji vivuko vingine vingi zaidi, tuna Sh3.7 bilioni kwa ajili ya kivuko kingine cha Dar es Salaam,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Ufundi na Umeme
Tanzania (Temesa), Mhandisi Marcellin Magesa alisema mradi wa ujenzi wa
kivuko cha Dar es Salaam – Bagamoyo ulianzishwa na Serikali kupitia
bajeti yake ya mwaka 2013/14.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment