Pages

Thursday, November 13, 2014

ULIMWENGU: NI AIBU KWENDA KUTIBIWA NJE

Ulimwengu: Ni aibu kwenda kutibiwa nje
MCHAMBUZI wa masuala ya siasa na kijamii, Jenerali Ulimwengu, amesema ni kitendo cha aibu kwa viongozi wa Bara Afrika kwenda kutibiwa nje ya nchi magonjwa madogo ambayo yangeweza kutibiwa katika nchi zao.

Ulimwengu, aliyasemwa hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), huku akibainisha kuwa, viongozi wengi wa bara hilo hupenda kwenda kupata matibabu nje ya nchi zao pindi wanapoumwa.
Alisema hali hiyo ya viongozi wa Afrika kukimbilia nje ya nchi kwenda kupata matibabu ni kunatokana na ukweli kwamba, wameshindwa kutengeneza mfumo bora wa afya ambao ungeweza kutoa tiba hata kwa wagonjwa kawaida.
“Mazingira hayo, ndiyo yanawafanya viongozi wengi wa bara hilo wakimbilie katika nchi za magharibi au Marekani kwa ajili ya kupata matibabu,” alisema Ulimwengu.
Alisema wakati mwingine matatizo yanayowapeleka huko nje ni ya kawaida, lakini kwa sababu nyumbani kwao hawajaweka mpangilio, vifaa na wataalamu ambao wangeweza  kuwahudumia matatizo kama hayo, hivyo wanaona ni heri waende huko.
Ulimwengu, alisema kwenda kwao kutibiwa huko nje, kunawafanya wajione kuwa watakuwa salama zaidi.
“Hii ni aibu kwa Bara la Afrika, kwa mfano maradhi mengine ni madogo sana na matibabu yake yanaweza kufanyika hapa Afrika,” alisema Ulimwengu.
Alisema pamoja na kwamba wataalamu wapo katika bara hilo, lakini bado wakuu hao wanakwenda kufanyiwa upasuaji mdogo katika nchi za Ulaya na Marekani.

CHANZO: TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment