
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai (kulia) akiwakabidhi ripoti ya
akaunti ya Escrow, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), Zitto Kabwe (katika) na makamu wake Deo, Bungeni mjini
Dodoma jana.
Bunge jana lilikabidhi ripoti ya
uchunguzi wa IPTL kwa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ili ipitie na
kutoa mapendekezo bungeni, hatua ambayo inatazamiwa kusababisha
mtikisiko wa tano katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete.
Ripoti hiyo iliyoandaliwa na Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), katika vitabu vitano, ilikabidhiwa na
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kwa Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe huku
akimpa masharti ya kuipitia kwa siri, kinyume na Zitto alivyokuwa
ameahidi kuwahoji watuhumiwa katika kikao cha wazi.
Ripoti hiyo inatokana na uchunguzi maalumu wa
fedha zilizochotwa katika akaunti ya escrow ndani ya Benki Kuu ya
Tanzania (BoT), iliyokuwa inatunza fedha za gharama za uwekezaji
(capacity charge) kwa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL baada ya kutokea
mgogoro wa kibiashara baina yake na Tanesco.
Tanesco ililalamika kuwa ilikuwa inailipa zaidi
IPTL kinyume na gharama za uwekezaji hivyo kuamuliwa na Mahakama kuwa
fedha ilizokuwa inatakiwa kulipa ziwekwe katika escrow hadi upatikane
ufumbuzi wa mgogoro huo.
Hata hivyo, kesi hiyo ilipohukumiwa Februari mwaka
huu, ikibainisha kweli Tanesco ilikuwa inailipa zaidi IPTL, ilibainika
kuwa fedha zilizokuwa katika akaunti hiyo Sh 306 milioni
zilikwishachotwa na IPTL kwa ruksa ya baadhi ya viongozi wa Serikali.
Kutokana na hali hiyo, ripoti hiyo inaweza
kuondoka na vigogo waliohusika na kashfa hiyo, kama ilivyowahi kutokea
katika kashfa nyingine nne zilizoitikisa Serikali ya Awamu ya Nne ya
inayoongozwa na Rais Kikwete
Richmond
Kashfa kubwa iliyotikisa nchi katika kipindi cha
awali cha Rais Kikwete ilikuwa ni Richmond ya mwaka 2006. Hii ilitokana
na tatizo kubwa la uhaba wa umeme na Serikali kulazimika kutafuta njia
za dharura za kutatua tatizo hilo, zikiwamo zilizodaiwa kukiuka taratibu
na sheria.
Baada ya kashfa hiyo kuchunguzwa na taarifa
kutolewa bungeni, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa alilazimika
kujiuzulu baada ya kutakiwa ajipime kutokana na mazingira ya kashfa
hiyo.
Wengine waliong’oka madarakani ni mawaziri wa Nishati na Madini kwa vipindi tofauti, Nazir Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha.
EPA
Mwaka 2008 iliibuka kashfa nyingine ya wizi wa
mabilioni katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (Epa) katika BoT na
vigogo kadhaa walitumia mbinu chafu kuchota zaidi ya Sh133 bilioni
katika akaunti hiyo.
Katika wizi huo ulioitikisa nchi, wahusika
walitajwa kutumia vivuli vya siasa kupitisha nyaraka bila kufanyiwa
uhakiki. Ilimalizika kwa baadhi yao kufikishwa mahakamani na wengine
ambao hawakutajwa kusamehewa na Rais Kikwete wakidaiwa kurejesha fedha
walizoiba.
Katika kipindi hicho, yalipofanyika mabadiliko
ndani ya Baraza la Mawaziri aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakia Maghji
hakurudi huku Gavana wa BoT, Daudi Balali akitimuliwa.
Ripoti ya CAG 2012
Mei 2012 ilipotolewa Ripoti ya CAG na kujadiliwa bungeni, ulitokea mtikisiko mkubwa uliowang’oa mawaziri sita na manaibu wawili.
Waliong’olewa ni Dk Cyril Chami (Viwanda na
Biashara), Omary Nundu (Uchukuzi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii),
Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Mustafa Mkulo (Fedha) na
William Ngeleja (Nishati na Madini) na manaibu waziri wawili; Athumani
Mfutakamba (Uchukuzi) na Dk Lucy Nkya (Afya).
Operesheni Tokomeza Ujangili
Mwishoni mwaka jana, matokeo ya Operesheni
Tokomeza Ujangili (Otu), iliyoanzishwa na Serikali nayo ilizua mtikisiko
mwingine uliowang’oa madarakani mawaziri wanne ambao wizara zao
zilielezwa kushindwa kusimamia vizuri utekelezaji wa operesheni hiyo.
Mawaziri waliong’olewa ni Khamisi Kagasheki wa
Maliasili na Utalii, Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi),
Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Waziri wa
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.
PAC yapewa rungu
Katika makabidhiano ya ripoti yaliyoshuhudiwa na
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge),
William Lukuvi na wajumbe wengine watatu wa PAC, Ndugai alisema;
“Naielekeza kamati yako ifanye uchambuzi na kutoa maoni na mapendekezo
katika kila hadidu rejea.
“Katika kufanya uchambuzi kamati ijikite zaidi katika kufanya uchambuzi wa CAG na Takukuru.”
Ndugai alisema katika uchunguzi wake, CAG
aliwahoji wote waliohusika na jambo hilo na kisha kuwasilisha taarifa
yake kwa Takukuru kwa hatua zaidi.
“Kamati ifanye kazi kwa kuzingatia kanuni ya tatu
na nne kwa kuzingatia nyongeza ya saba ya kanuni za Kudumu za Bunge za
mwaka 2014 na kifungu cha tisa kifungu kidogo cha kwanza na cha 31 vya
Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge, Sura ya 299,” alisema.
Alisema ni matumaini yake kwamba baada ya kumaliza
kazi ya kutoa maoni na mapendekezo, taarifa iwasilishwe kwake (Ndugai)
ili ajiridhishe kabla ya kuwasilisha bungeni.
“Nimemwelekeza Katibu wa Bunge, asimamie na awape
ushirikiano unaotakiwa ili kazi yenu iweze kuwa ya ufanisi na yenye
kiwango,” alisema.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah aliikabidhi PAC watendaji wanne ambao wataisaidia kufanya kazi hiyo.
Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Zitto
alisema kamati yake itazingatia maagizo ya Ndugai kutokana na masuala ya
kimahakama yaliyomo ndani ya ripoti hiyo.
“Kwa hiyo PAC haitakuwa na utaratibu wa kawaida
ambao tunafanya tunapowaita watu wakati wa kuhoji mahesabu yao.
Nimeshtuka kidogo maana Bunge limeipa nguvu sana PAC katika jambo hili
kwa kuwaelekeza kutumia sheria namba tatu. Sisi tutaitumia nguvu hiyo
kutenda haki katika jambo hili zima, haki kwa Watanzania na watu ambao
wametajwa kuhusika katika jambo zima.”
Zitto alisema ripoti hiyo inaonyesha jinsi taasisi
za kiuwajibikaji zinavyofanya kazi, mambo ambayo huwezi kuyaona katika
nchi nyingine.
“Bunge liliagiza kupitia kamati yake ya PAC tangu Machi, 20
2014, baada ya kuona taarifa hiyo katika Gazeti la The Citizen,
tukachukua hatua na kuagiza ukaguzi ufanyike. Baadaye jambo hili
likaibuka bungeni, Waziri Mkuu (Mizengo Pinda) alipojibu hoja ya
mheshimiwa (David) Kafulila, akaagiza tusubiri uchunguzi ambao PAC
umeagiza.”
Alisema jambo hilo linajenga imani kubwa kuwa nchi
inaendeshwa kwa taratibu na imeondoa hofu ya baadhi ya watu kuwa
taarifa hiyo haitafika katika kamati kujadiliwa.
Alisema kwa msingi huo, Bunge linajaribu kukwepa mbinu zinazoweza kutumiwa na watu kuzuia kupelekwa mahakamani.
Akizungumzia wafadhili ambao wamejitoa kusaidia
nchi, Zitto alisema; “Uhusiano kati yao na Serikali ni wao, sisi PAC
hatuwezi kuwasemea. Bunge linasimamia uwajibikaji lakini kwa vyovyote
vile kama wasiwasi wao ulikuwa ni taarifa ya PCCB na CAG kutofanyiwa
kazi mmeona dhahiri hapa kwamba tumeifanyia kazi.”
Alipoulizwa iwapo siku 10 zinatosha kukamilisha
kazi, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe alisema ni nyingi kwa
sababu kamati hiyo ni makini na ina wataalamu waliobobea.
The Citizen lasifiwa
“Nataka nikiri bayana hata sisi PAC tulikuwa
hatujui kama fedha hizi zimechotwa, it was just one paper, The Citizen
(ilikuwa ni gazeti moja) waliandika investigative story (habari ya
uchunguzi), mwenyekiti wangu (Zitto) aliiona akaileta kwenye kamati
tukamuita Gavana akathibitisha ni kweli fedha zimechotwa,” alisema
Filikunjombe.
Alisema kamati ilichukua hatua na kutaka waandishi wa habari kujivunia kazi yao nzuri waliyoifanya kwa kuwa ni mafanikio yao.
IPTL waibuka
Baada ya kukabidhiwa kwa ripoti hiyo jana katika
Viwanja vya Bunge, alionekana Meneja Uhusiano wa IPTL, Sylvester Joseph
ambaye alisema amefika hapo kufuatilia kama ripoti hiyo imewasilishwa na
akasema kampuni hiyo itatoa ushirikiano kwa Bunge itakapohitajika
kufanya hivyo.
CHANZO: MWANANCHI
Membe na wafadhili
Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema leo anatarajia kukutana
na wahisani waliogoma kutoa misaada inayofikia Dola 560 milioni za
Marekani kwa Serikali kutokana na kashfa ya IPTL.
Membe aliyasema hayo Dar es Salaam jana baada ya
kufungua mkutano wa kwanza wa kimataifa wa Sauti ya Sayansi ya Jamii,
unaokutanisha wasomi kutoka Afrika, akisema wahisani hao walitaka
Serikali kuchukua hatua dhidi ya kashfa hiyo ya IPTL ambayo tayari
imechukuliwa.
“Waligoma kutoa misaada hiyo hadi waone Ripoti ya
CAG, sasa tayari imetoka, hivyo nitakutana nao kesho (leo) ili niweze
kujua wanasemaje, bado wataizuia au watatoa?”
Alisisitiza kuwa uamuzi huo wa wahisani umeathiri
kwa namna fulani utekelezaji wa Bajeti ya Serikali, hivyo hatua kali
zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo.
“Hatuwezi kuacha kuchukua hatua tukikuta madudu
humo kwenye Ripoti ya CAG kwa sababu imetugharimu, hatuko tayari
kuzikosa fedha hizo za wahisani,” alisema.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment