Pages

Wednesday, November 19, 2014

MOTO WATEKETEZA MADUKA 180 JIJINI ARUSHA

Mmoja wa wafanyabiashara ambaye moja ya duka lake kati ya 180 yaliyoteketea kwa moto jijini Arusha usiku wa kuamkia jana, akiangalia mabaki ya vitu vilivyoungua.
Maduka 180 ya kuuza vitu mbalimbali kwa watalii yaliyopo eneo la Mount Meru, jijini Arusha yameteketea kwa moto.
Maduka hayo yaliyoko Curions jirani na ofisi za CCM Wilaya ya Arusha na ofisi za Zimamoto, yaliteketea kwa moto juzi usiku.
Akizungumza jana katika eneo la tukio, Mwenyekiti wa soko hilo, Mussa Kakulula, alisema moto huo ulizuka saa 3:00 usiku baada ya maduka hayo kufungwa.Kakulula alisema kwa kawaida, maduka hayo hufungwa saa 12:00 jioni na kufunguliwa asubuhi.
Alisema moto huo uliteketeza vitu vyote na hakuna kilichookolewa licha ya kuwa mita chache na kituo cha zimamoto. Kakulula alisema walijaribu kuokoa mali zote zilizokuwa ndani,  lakini kila walipokuwa wakizitoa nje ziliporwa na vibaka.
Kadhalika, Mwenyekiti huyo alisema kwamba sababu nyingine iliyosababisha mali hizo kuteketea ni wafanyakazi wa Idara ya Zimamoto kuchelewa kufika eneo hilo.
Kakulula alisema wanashindwa kuelewa chanzo cha moto huo kwa kuwa soko hilo halina umeme. Kuhusu hasara iliyotokana na moto huo, alisema hawajajua thamani halisi ya mali iliyoteketea.
Hata hivyo, alisema mfanyabiashara mwenye mtaji mkubwa alikuwa na mtaji wa takribani Sh. milioni 70 na mwenye mtaji mdogo Sh. milioni 15 na kwamba wote walikuwa wakiuza mali zao na kuacha fedha katika eneo hilo kutokana na kuwa na usalama.
Naye Katibu Msaidizi wa soko hilo, Godfrey Emmanuel, alisema kuwa baada ya moto kuzuka, waliwapigia watu wa Zimamoto, lakini walichelewa kufika na hata walipokwenda, gari lao halikuwa na maji.
Alisema walichofanya ni kuzima moto ili usienee nyumba za jirani, lakini eneo lote la soko lilikuwa tayari limekwishateketea.
Kwa upande wake, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, alisema kuwa watu wa Zimamoto wanapaswa kuadhibiwa kutokana na kushindwa kutimiza jukumu lao.
Mulongo ambaye bado hajakabidhi ofisi kwa mrithi wake, Evarist Ndikilo, alisema Zimamoto wanastahili adhabu kwa kuwa ofisi zao ziko mita chache na eneo hilo, hivyo hapakuwapo na sababu ya kuchelewa na kuudhibiti moto huo.
Aliongeza kwamba licha ya kushindwa kuudhibiti moto huo, wafanyakazi wa Zimamoto wametia aibu kwani walipofika bado hawakuwa na maji.Aliwapa pole wafanyabiashara hao ambao wengi wao walikuwa wakiuza vinyago na bidhaa za shanga na nguo za utamaduni.
Mulongo alisema atajitahidi kutafuta wadau ili wachangishane na kurejesha haraka hali ya soko hilo ambalo kwa kiasi kikubwa linategemewa na watalii wanaofika mkoani hapa.
Naye mmoja wa wafanyabiashara katika soko hilo, Bariki Ngowi, alisema hadi sasa amechanganyikiwa kwani alikopa fedha za kununulia mzigo mkubwa wa mali kwa ajili ya kuuza wakati wa sikukuu ya Krismasi.
“Lakini sasa sijui nitalipaje fedha hizo, maana vitu vyote vimebaki majivu tu, yaani sina hata la kufanya, nimevunjika moyo,” alisema huku akitikisa kichwa bila kutaja alikopa wapi fedha hizo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment