Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (pichani), alitoa kauli hiyo bungeni jana akisema taifa limepoteza watu 17, katika matukio matatu yaliyotokea Januari na Novemba Mwaka huu, katika vurugu baina ya wakulima na wafugaji.
Alisema serikali ya Wilaya ya Kiteto itaimarishwa ili iweze kukabiliana na migogoro inayojitokeza kikamilifu,kwa kufanya mabadiliko ya uongozi, katika ngazi mbalimbali za utawala, ndani ya Wilaya na Mkoa, haraka itakavyowezekana, ndani ya wiki hii.
“Lakini naomba vilevile nitangulize kuomba radhi kwa sababu jambo hili matukio yameanza kuhusisha hata matumizi ya silaha za kisasa kutoka zile za jadi,” alisema.
Alisema Novemba 11, mwaka huu wafugaji waliingiza mifugo kwenye shamba la mihogo la Mzee Hassan (65), ambaye baadaye alitekwa na kuuawa wakati akifuatilia haki yake na mwili wake kupatikana kesho yake ukiwa umetupwa vichakani.
Pinda alisema tukio hilo lilifuatiwa na mauaji ya kulipiza kisasi kati ya wakulima na wafugaji na kuwa jumla ya watu watano na kutokea uharibifu wa mali.
Alitaja majina ya waliouawa katika tukio hilo, kuwa ni Mzee Hassa (65), mkulima - Mrangi, Maria (35)-Mmasai, Job Nsavu (48) Mgogo, Julius Andrea (52)-Mrangi na Mmasai mmoja ambaye jina lake halikuwa limetambulika.
Wakati juhudi za kurejesha amani katika eneo la Matui, Pinda alisema vurugu nyingine zilijitokeza Novemba 13, 2014 katika Kijiji cha Chekanao na Wazee wawili wakulima kuuawa na maboma ya kimasai 13 yakachomwa moto.
Alisema mpaka jana, jumla ya watu 13 walikuwa wametiwa mbaroni na kwamba watafikishwa mahakamani leo.
Waziri Pinda alisema, pamoja na hatua nyingine zinazochukuliwa kwa lengo la kukomesha matukio hayo, Serikali inaendelea kufuatilia kuona kuwa viongozi wa kiserikali na kisiasa, wanatatua migogoro ya kijamii, badala ya kuitumia kwa manufaa yao.
Alisema matukio hayo ni muendelezo wa tukio la Januari 12, 2014 ambapo kundi la wafugaji wa Kimasai wapatao kati ya 40 hadi 50 waliendesha mashambulizi ya kushtukiza, wakitumia silaha za moto na kusababisha vifo vya watu 10 huku mabanda 60, pikipiki sita na baiskeli 53 vikichomwa moto.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment