Pages

Wednesday, November 19, 2014

MAMEYA KUTOKA NCHI 25 DUNIANI KUKUTANA DAR

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Massaburi
Zaidi ya Mameya 50, maofisa mipango miji na wataalam mbalimbali kutoka majiji 25 duniani, wanakutana jijini Dar es Salaam katika mkutano wenye kaulimbiu `Fikiri nje ya mipaka yako' na kubadilishana uzoefu katika kusimamia ukuaji haraka wa miji kupitia mpango ya mji mkuu.  Mkutano huo unaojulikana kama Global Lab, umeandaliwa kwa ushirikano wa Benki ya Dunia na Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Philippe Dongier, alisema Jiji la Dar es Salaam ni miongoni mwa majiji yanayokuwa kwa kasi duniani na kwamba ukuaji huo unapaswa kuwekewa mazingira rafiki ya ukusanyaji kodi, kurekebisha mipangilio ya utawala ili kuwezesha upangaji wa mji, ukuaji wa viwanda na huduma muhimu za kijamii.
Aliongeza kuwa ongezeko hilo linapaswa kuwezesha ushindani wa biashara zinazozalisha ajira zenye tija.
Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Didas Massaburi, alisema MetroLab, inalenga kuhakikisha ufanisi wa mipango miji kwa manufaa ya wakazi wake, kwenye sekta za uchumi, shughuli za kijamii na mazingira.
Katika mkutano huo wa siku tatu, washiriki watajadili namna ya kuhakikisha ukuaji wa miji na majiji unakuwa endelevu kwa kuhakikisha huduma muhimu kama usafiri na miundombinu, ardhi, makazi, upatikanaji wa maji safi, udhibiti wa maji taka na takataka nyingine.
MetroLab ni mpango uliozinduliwa Aprili, mwaka jana jijini New York na unaweka utaratibu wa majiji kubadilishana ujuzi na uzoefu ili kukabiliana na ukuaji wa kasi wa miji.
Washiriki wa mkutano huo wanatoka majiji ya Accra, Addis Ababa, Arusha, Colombo, Dar es Salaam, Ilala, Ilemala, Kaduwela, Kigali, Kisumu, Kinondoni, Mbeya, Moratuwa, Mumbai, Mwanza, Nairobi, New York, Paris, Karachi, Seoul, Rio de Janeiro, Singapore, Tanga, Temeke na Zanzibar.
Washiriki hao watatembelea miundombinu ya mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Massaburi amesema fedha zimekwamisha kuhama kwa Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani Ubungo (UBT) huku akisisitiza kuwa mpango wa kukihamisha bado upo.
Alisema tayari upembuzi yakinifu umekwishafanyika na kwamba jiji limepata Sh. bilioni 30 kutoka Benki ya Rasilimali (TIB) ambazo hata hivyo amesema hazitoshi kwa kuwa mradi huo unahitaji Dola za Marekani milioni 150.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment