Vurugu hizo zilizoanza saa 6:30 mchana, zilisimamisha shughuli za wafanyabiashara katika mitaa ya Lumumba, Rwagasore, Market, Pamba, Nyerere na kituo cha Chai na Soko Kuu.
Vurugu hizo zilisababisha makundi ya wananchi waliokuwa wakipita ama kufanya shughuli mbalimbali za kujipatia kipato kuikimbia mitaa hiyo ili kunusuru maisha yao, huku wengine wakipoteza mali zao.
Machinga hao waliharibu kwa kuvunja vioo vya Msikiti wa Masingasinga wa Gurudwara Siri Guru Singh Sabha uliopo kati ya mtaa wa Lumumba na Market, jijini hapa. Vurugu hizo zilianza baada ya askari wa jiji hilo kuwaondoa Machinga hao katika mitaa wasiyoruhusiwa kufanya biashara zao na walipozidiwa nguvu waliomba msaada kwa polisi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, alisema waliamua kutumia FFU kutuliza vurugu hizo baada ya kuombwa na jiji baada ya mgambo wake kuzidiwa nguvu na Machinga hao.
“Ni operesheni ya kawaida ya jiji ya kuwaondoa Machinga katika mitaa isiyoruhusiwa, tumesaidia kuongeza nguvu ili kudhibiti vurugu hizo,” alisema Kamanda Mlowola.
Hata hivyo, Kamanda Mlowola hakutaka kuingia kwa undani kuhusiana na tukio hilo ikiwamo idadi ya Machinga waliokamatwa na polisi na uharibifu wa mali.
Alisema tu Wamachinga kadhaa walitiwa mbaroni na kwamba walikuwa wakiendelea kuwadhibiti katika maeneo yote ya jiji ambayo yalikumbwa na vurugu hizo.
NIPASHE ilijaribu kumtafuta Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga, kuzungumzia vurugu hizo, lakini hakupatikana kupitia simu yake ya mkononi.
Kama ilivyokuwa kwa Konisaga, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Hassan Hida, hakupokea simu ya mwandishi.
Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoani Mwanza, Christopher Wambura, alisema kutokana na vurugu za wafanyabiashara hao maduka ya wafanyabiashara wakubwa yalifungwa kuepusha uwezekano wa vitendo vya uporaji.
“Machinga hawa wamesaba bisha maduka kufungwa hali iliyowatia hasara wafanyabiashara wetu, lakini kuna hasara kubwa zilizosababishwa na vurugu hizo,” alisema Wambura.
Wambura alisema umoja wa wafanyabiashara hao utatoa tamko leo kuhusiana na vurugu hizo.
Vurugu hizo zimetokea siku tano baada ya kutokea vurugu nyingine kama hizo na kutulizwa na FFU.
Jiji la Mwanza limekuwa likigubikwa na vurugu za mara kwa mara kati ya Machinga, mgambo wa jiji na FFU, kuhusiana na maeneo ya kufanyia biashara zao mtaani.
     CHANZO:
     NIPASHE
    


No comments:
Post a Comment