Pages

Friday, November 21, 2014

MACHINGA 25 WAKAMATWA KWA VURUGU

Kamanda wa polisi mkoani Mwanza,Valentino Mlowola.
Wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu machinga 25, wamekamatwa na Jeshi la Polisi miongoni mwao wamefikishwa mahakamani kwa kosa la uharibifu gari la Halmashauri ya Jiji la Mwanza na msikiti wa masingasinga wa Gurudwara Siri Guru Singh Sabha.
Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Valentino Mlowola, alisema machinga hao wamekamatwa kutokana na vurugu zilizotokea juzi na kutulizwa na askari wa FFU.
“Watu hao wamekamatwa kutokana na uharibifu wa vioo vya gari la Jiji na vioo vya msikiti huo…wapo waliofikishwa mahakamani leo (jana) kuhusiana na matukio hayo,” alisema Mlowola.
Hata hivyo,  Mlowola alisema bado jeshi hilo linaendelea kufanya tathmini zaidi ya mali zilizoharibiwa kutokana na vurugu hizo.
Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula, alipoulizwa na NIPASHE kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno, alijibu ‘nipo kikaoni’.
Lakini mkurugenzi wa jiji hilo, Halfa Hida, alipopigiwa simu alisema yuko Dodoma, hivyo hawezi kuzungumzia suala hilo zaidi ya kaimu wake ambaye hata hivyo hakuweza kupatikana kwa simu yake ya mkononi.
Machinga hao juzi walipambana na mgambo wa jiji kutokana na kugomea kuondolewa katika sehemu walizokuwa wakifanya biashara, hali iliyosababisha FFU kuingilia kati kudhibiti vurugu hizo.
Vurugu hizo zilitawala zaidi katika mitaa ya Rwagasore, Market, Pamba, Lumumba na kituo cha zamani cha mabasi maarufu Tanganyika.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment