
Viongozi wa vyama na Serikali nchini Tanzania ambao majina yao yanatajwa
na wananchi kuwa wanaweza kuwania nafasi ya urais kwenye uchaguzi mkuu
mwakani.
Kumekucha. Pengine hilo ndilo
neno linalofaa kutumika kuelezea matokeo ya utafiti kuhusu
kinyang’anyiro cha urais katika Uchaguzi Mkuu 2015 ambayo yanaonyesha
kuwa iwapo ungefanyika leo, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
angeibuka mshindi.
Wakati Lowassa angeibuka na ushindi kwa asilimia
13 na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda angefuatia kwa karibu akiwa na asilimia
12 huku Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akiwa wa tatu kwa
asilimia kumi na moja.
Hata hivyo, asilimia 33 ya wananchi waliohojiwa walisema bado hawajaamua wampigie kura mgombea gani.
Utafiti huo wa Taasisi ya Twaweza unayoonyesha
wagombea hao kukabana kwa tofauti ya asilimia mojamoja na ambao
ulitangazwa Dar es Salaam jana, ulifanywa Septemba 2014 kwa kuwahoji
wananchi 1,445 kutoka Tanzania Bara.
Akitangaza matokeo hayo, mtafiti wa Twaweza, Elvis
Mushi alisema utafiti huo ni wa tatu kufanyika nchini na kwamba awamu
ya kwanza ilifanyika mwaka 2012 na Lowassa alipata asilimia sita kabla
ya mwaka jana na mwaka huu kuibuka na asilimia 13.
Akimzungumzia Pinda, mtafiti huyo alisema mwaka
2012 alipata 16, lakini zilishuka mwaka 2013 hadi kufikia asilimia kumi
na moja na kupanda tena mwaka huu hadi 12.
“Kwa upande wa Dk Slaa, mwaka 2012 na 2013 alipata asilimia 19 lakini sasa ameshuka hadi asilimia kumi na moja,” alisema Mushi.
Wagombea wengine waliotajwa na asilimia zao kwenye
mabano ni Profesa Ibrahim Lipumba (6%), Dk John Magufuli (3%), Freeman
Mbowe (3%), Samuel Sitta (4%), Bernard Membe (5%) na Zitto Kabwe (1%).
“Hata hivyo, kitu muhimu cha kuangalia katika
ripoti hii siyo tu majina ya mgombea, bali ni idadi ya wananchi asilimia
33 ambao wamesema hawajui watamchagua nani,” aliongeza Mushi.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa iwapo vyama vyote vya
upinzani vitaungana na kumchagua mgombea urais mmoja, asilimia 41 ya
wananchi waliohojiwa walisema wangemchagua Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willibrod Slaa, akifuatiwa na Profesa Lipumba (14%), Mbowe (11%) na
Zitto Kabwe (6%).
Wanasiasa wengine waliotajwa ni Tundu Lissu,
Maalim Seif Sharif Hamad, James Mbatia na Augustino Mrema ambao kila
mmoja aliambulia asilimia moja.
Wengi kuchagua CCM
Pia utafiti unaeleza kuwa iwapo Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) utasimamisha mgombea mmoja wa urais dhidi ya CCM, asilimia 47 ya
wananchi walisema wangeichagua CCM huku asilimia 28 wangempigia kura
mgombea wa muungano wa upinzani. Asilimia 19 ya wananchi walisema
watampigia kura mgombea bila kujali chama chake.
“Kura za kundi hili zitategemea ubora wa wagombea.
Kama kura hizo zitagawanywa kwa CCM na upinzani, CCM itashinda urais
kwa kuzidi upinzani kwa kura nyingi kiasi. Kutakuwa na kitisho kwa
ushindi wa CCM endapo wapigakura wote watamchagua mtu badala ya chama
watampigia mgombea wa upinzani, kitu ambacho kina uwezekano mdogo
kutokea,” inasema ripoti hiyo.
Wananchi walia uchumi, afya na elimu
Wananchi walipoulizwa ni matatizo gani matatu
makubwa yanayoikabili Tanzania walitaja ukosefu wa elimu bora, afya na
hali mbaya ya kiuchumi na kwamba matatizo hayo yameshika nafasi ya juu
kwa miaka mitatu mfululizo.
“Umaskini umeongezeka kutoka asilimia 49 mwaka
2012 hadi 63 mwaka 2014, huku matatizo ya afya yakiongezeka kutoka
asilimia 40 hadi 47 na elimu imeshuka kutoka asilimia 46 mwaka jana hadi
38 mwaka huu,” alisema Mushi.
Wabunge na ahadi zao
Katika utafiti huo, imeelezwa kuwa ahadi nyingi
zilizotolewa na wabunge kwenye mikutano ya kampeni wakati wa uchaguzi
hazijatekelezwa na kwamba asilimia 78 ya wananchi bado wanazikumbuka.
Ahadi nyingi zilizotolewa na wagombea zilihusu
miradi ya ujenzi barabara, maji, ujenzi wa hospitali, kuboresha elimu,
umeme, mikopo kwa vikundi, kuongeza ajira, kujenga madaraja na kuboresha
kilimo.
Pia ripoti imeweka wazi kuwa karibu nusu ya
wabunge wote huenda wasirudi tena katika nyadhifa zao. Asilimia 47 ya
wananchi walioulizwa iwapo watampigia tena kura mbunge wao walisema
hapana huku asilimia kama hiyo wakisema ndiyo.
Akizungumzia utafiti huo, mwandishi wa habari
mkongwe nchini, Jenerali Ulimwengu alihoji namna majina ya wagombea
yaliyotajwa kwenye ripoti hiyo yalivyopatikana huku akipendekeza namna
sahihi ya kuwalinganisha wagombea hao.
“Walitakiwa kulinganishwa kwa mfano kwenye kilimo,
watuambe Mizengo Pinda anaweza kufanya nini akilinganishwa na mgombea
mwingine. Vinginevyo inakuwa ni mashindano ya urembo. Tunatumia muda
mrefu kumchagua mbuzi Vingunguti kumbe atachinjwa kesho,” alisema
Ulimwengu.
Kwa upande wake, Dk Benson Bana wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, alisema hatashangaa kusikia kuna watu wengine wametoa
ripoti nyingine kupinga utafiti huo kwa kuwa kumekuwapo na utamaduni wa
kutokukubaliana na matokeo ya namna hiyo.
Kauli ya Nape
“Tafiti hupingwa na tafiti, kwa hiyo mtu asianze kupinga tu,
fanya kama wao (Twaweza) jifunze kutumia takwimu,” alisema huku
akionyesha kukasirishwa na watu waliokuwa wakitoa maoni ya kupinga
ripoti hiyo.
Kauli ya Nape
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
alisema anakubaliana na matokeo hayo kwa kuwa yamepatikana na njia ya
simu katika nchi ambayo ina watumiaji wengi wa aina hiyo ya mawasiliano.
Hata hivyo, alisema: “Tatizo ahadi nyingi
zinazotolewa na viongozi kwa wananchi hazitekelezwi. Tunasema asilimia
80 ya Watanzania ni wakulima lakini asilimia mbili ya viongozi ndiyo
walioahidi kuhusu kilimo.”
Mjumbe wa lililokuwa Bunge la Katiba, Maria
Sarungi alisema ripoti hiyo haina habari njema kwa vyama vya siasa kwa
sababu inaonyesha kuwa wananchi wamekosa imani ya kupata msaada, badala
yake wameanza kumtafuta ‘mkombozi’ atakayewasaidia.
“Inapotokea asimilia 41 wanasema hawajui
watamchagua nani huku asilimia 10 wakisema inategemea na mtu
atakayejitokeza inaonyesha wananchi wanamtafuta mtu atakayewasaidia na
siyo chama.
“Mambo ya wananchi yanatatuliwa na Katiba, tatizo la utawala bora na umaskini haliletwi na vyama vya siasa linaletwa na Katiba.”
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment