Wananchi wapikita jirani na bango linaloonyesha viwango vya kubadilishia
fedha za kigeni katika moja ya maduka ya katika Mtaa wa Samora Avenue,
jijini Dar es Salaam.
Hatua ya wahisani kuzuia Sh1 trilioni za misaada ya kibajeti kwa Serikali kutokana na kashfa ya IPTL na wasiwasi wa Uchaguzi Mkuu mwakani, ni miongoni mwa sababu za kuporomoka kwa kasi thamani ya Shilingi nchini, imefahamika.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wiki iliyopita,
wasomi na wadau wa biashara nchini walisema sababu nyingine ni uagizaji
na uuzaji bidhaa nje ya nchi.
Kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) Januari 2, mwaka huu, Dola moja ya Marekani ilikuwa ikiuzwa kwa
Sh1,586 lakini sasa imepanda hadi Sh1,745. Ikumbukwe kuwa katikati ya
mwaka huu, Dola moja ilikuwa ikinunuliwa kwa hadi Sh1,800 katika baadhi
ya benki na maduka ya kubadilishia fedha, jambo lililoongeza gharama za
ufanyaji biashara na kuongeza bei ya bidhaa.
Escrow
Hivi karibuni, wahisani walitangaza kusimamisha
misaada hadi Serikali itakapopitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow na
kuchukua hatua.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk
Prosper Ngowi alisema hatua iliyochukuliwa na nchi wahisani ya kuzuia
fedha za misaada hiyo ambazo zingeingia katika mzunguko wa fedha,
imesababisha upungufu wa Dola katika soko la fedha, hivyo kuongezeka
thamani.
Alisema iwapo fedha hizo zingekuwa kwenye
mzunguko, zingesaidia kupunguza uhaba wa Dola uliopo ambao umesababisha
kuuzwa kwa bei kubwa na hivyo kuchangia kupandisha thamani ya Shilingi.
“Hata kitendo cha Tanzania kuuza bidhaa chache nje
ya nchi kimechangia mahitaji ya Dola kuongezeka kutokana na uhaba wa
fedha hizo hapa nchini,” alisema Dk Ngowi akitaja sababu nyingine ya
kuporomoka kwa Shilingi.
Hoja ya Dk Ngowi iliungwa mkono na Meneja wa Fedha
wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Mshindo Ibrahim akisema kuzuiwa
kwa fedha hizo za hisani, kumechangia kupaisha thamani ya Dola, licha
ya kuwapo tatizo la kuuza bidhaa kidogo nje ya nchi.
“Sisi ni waagizaji wakubwa wa bidhaa kuliko kuuza
nje, tunajikuta tunapata Dola kidogo kuliko mahitaji jambo linaloiongeza
thamani yake, lakini hili la wahisani kushikilia fedha za bajeti
kutokana na sakata la IPTL ni moja ya sababu kubwa kwa sasa,” alisema
Ibrahim.
Iwapo wahisani ambao hutoa fedha zao kwa sarafu za
kigeni wataziachia, mtaalamu huyo alisema zitasaidia kupunguza wingi wa
Shilingi kwa kuwa Dola hizo zinatakiwa kubadilishwa kwa sarafu ya ndani
ili zianze kutumika.
Alisema kuna wakati hali hiyo ni kawaida kibiashara.
Uchaguzi Mkuu
Uchaguzi Mkuu
Katika hatua nyingine, Ofisa Mtendaji Mkuu wa
Kampuni ya Dhamana na Uwekezaji ya Zan Securities, Raphael Masumbuko
alisema safari hii Shilingi imeshuka thamani kwa kasi isiyo ya kawaida
tofauti na miaka ya nyuma, jambo ambalo linaweza kuchangiwa na homa ya
uchaguzi.
“Huenda imetokea kwa sababu tunaelekea katika
kipindi cha uchaguzi. Katika kipindi kama hiki, wawekezaji wengi kutoka
nje huwa wanahifadhi fedha zao katika Dola ili kujiokoa na hasara iwapo
utatokea mfumuko wa bei wakati wa mchakato wa uchaguzi,” alisema
Masumbuko.
Alisema Shilingi pia imeshuka thamani kutokana na
Dola kutumika mno katika sekta ya nyumba na msimu huu ni wa kulipa kodi,
hivyo Dola inahitajika zaidi kuliko Shilingi.
“Nyumba nyingi siku hizi zinakodishwa kwa Dola
wanaita ‘mita ya mraba kwa Dola’ hadi majumba yanayomilikiwa na mifuko
ya hifadhi za jamii… sasa kwa hali hii usitegemee Shilingi itapanda
thamani,” alisema Masumbuko.
Hata hivyo, alisema hali hii haitakiwi kutia hofu
Watanzania kwa kuwa inaweza kutengamaa baada ya msimu wa baridi kuanza
Ulaya ambako watalii wengi watakuja na kuleta fedha za kigeni, pia juzi,
BoT imeuza dhamana zitakazoipunguza Shilingi sokoni.
Mkuu wa Kitivo cha Biashara cha Chuo Kikuu cha
Tumaini Dar es Salaam, Deogratius Massawe alisema kuongezeka kwa bidhaa
mbalimbali nchini zinazonunuliwa kwa Dola pia kumechangia thamani ya
fedha hiyo kuongezeka huku Shilingi ikishuka.
Massawe alisema mfumo huo unawalazimisha
Watanzania kununua bidhaa hizo kwa bei ya juu zaidi tofauti na ile
inayouzwa kwa Shilingi.
“Hata hivyo, ipo sheria inayomzuia mtu
kumlazimisha mwingine kununua kitu chochote kwa Dola, ila mteja anaweza
kununua bidhaa kwa Dola iwapo wamekubaliana na muuzaji.”
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Benjamin
Mutagwaba alisema sera makini ndizo zinazoweza kuinusuru thamani ya
Shilingi ya nchi hii.
“Kama kutakuwa na usimamizi mzuri, kilimo pekee
kinaweza kuleta mapinduzi katika biashara na kubadili thamani ya
kubadili fedha. Kama mazao yote yataongezwa thamani kabla hayajauzwa
nje, nchi itapata fedha nyingi… unaweza ukaona hata madini
tunayasafirisha yakiwa hayajaongezwa thamani, jambo ambalo si zuri kwa
mustakabali wetu kiuchumi kama nchi,” alisema Profesa Mutagwaba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ukaguzi wa
hesabu ya KPMG, David Gachewa alisema hakuna njia ya mkato wa kuifanya
Shilingi iwe na thamani kama si kuongeza uuzaji wa bidhaa nje ya nchi.
“Miaka 10 iliyopita thamani ya Dola moja ya Marekani ilikuwa
Sh800 lakini leo hii ni Sh1,700 na bado tunaagiza bidhaa zilezile kwa
sarafu hiyo. Hii inamaanisha kuwa gharama za bidhaa hizo zimeongezeka na
mwananchi ndiye anayelipia. Hali hii itaendelea kama hakutakuwa na
mabadiliko ya kiuchumi ili kuongeza uuzaji wa bidhaa nje ya nchi,”
alisema Gachewa na kuongeza:
“Nadhani mafuta na gesi yatakapoanza kuzalishwa
hapa nchini na kusafirishwa kwenda nje itasaidia kwa kiasi kwa kuwa
Serikali itaokoa fedha zilizokuwa zinatumika kuagiza nishati hizo, pia
kuna fedha zitakazoingia kutokana na mauzo ya bidhaa hizo.”
Kauli ya waziri
Akijibu swali la Cecilia Pareso (Chadema - Viti
Maalumu) wiki iliyopita bungeni, kuhusu kuongezeka kwa matumizi ya fedha
za kigeni nchini, Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima alisema
linapunguza ufanisi wa sera za fedha na uwezo wa BoT kutimiza wajibu
wake kuwa mkopeshaji wa mwisho katika uchumi.
Malima aliongeza kuwa endapo wananchi watalazimika
kutumia fedha za kigeni, jambo hilo pia linaweza kuwa kero kwao kwa
kuwasababishia usumbufu.
Hata hivyo, Malima alisema kiwango cha matumizi ya Dola nchini hakijafikia kiasi cha kuwa na madhara hayo.
Alisema uwiano wa amana za fedha za kigeni na
ujazo wa fedha, ambao uliwahi kupanda hadi kufikia asilimia 34 mwaka
2003, kwa sasa umeshuka mpaka kufikia asilimia 27.2 mwaka 2013.
Alisema mwaka 2007, Serikali ilitoa tamko rasmi
kuhusu matumizi ya fedha za kigeni katika kulipia huduma na bidhaa
katika soko la ndani kuwa Mtanzania yeyote asilazimishwe kulipia huduma
au bidhaa yoyote kwa fedha za kigeni.
Baada ya agizo hilo, Malima alisema fedha za
kigeni zinazotunzwa na BoT ziliongezeka kutoka Dola 228.3 milioni mwaka
1993 sawa na asilimia sita ya Pato la Taifa hadi Dola 4 bilioni sawa na
asilimia 14 ya Pato la Taifa mwaka 2012.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment