Pages

Thursday, November 20, 2014

KAMATI YA ZITTO YAMHOJI CAG

Zitto Kabwe,Mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeanza kazi ya kuchambua ripoti za uchunguzi wa kashfa ya kuchota fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), huku ulinzi mkali unaohusisha askari wa Jeshi la Polisi wenye silaha za moto na makachero ukiwa umeimarishwa.
Mbali na kuchambua ripoti za uchunguzi huo uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), PAC inatumia fursa hiyo pia kuwahoji wahusika wote waliohojiwa na taasisi hizo wakati wa uchunguzi wao.
Habari za uhakika ambazo NIPASHE ilizipata mjini hapa jana zinaeleza kuwa wa kwanza kuhojiwa na PAC alikuwa ni Kaimu CAG, Francis Mwakapalila.
Mahojiano kati ya PAC na Mwakapalila yalianza saa tano asubuhi na hadi tunakwenda mitamboni yalikuwa bado yanaendelea.Ulinzi wa askari hao uliimarishwa siyo tu kwa watu baki, bali hata kwa wajumbe wa PAC.
Kila mjumbe wa PAC aliyefika katika ukumbi unaotumika kwa kazi hiyo, alikuwa akizima simu yake na kisha anaikabidhi kwa askari polisi, ambao pia walikuwa wanadhibiti hata wageni waliokuwa wakifika eneo la ukumbi wa kikao hicho.
Waandishi wa habari, ambao walifika jana katika jengo la Hazina, ambako PAC inalitumia kufanya kazi hiyo, kwa lengo la kufuatilia ahadi ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Zitto Kabwe, ya kuzungumza nao, lakini walizuiwa na askari hao.
Wakati wabunge hao wakitoa tuhuma hizo nzito kwamba serikali inatumia mahakama kuzuia Bunge kufanya kazi yake, hali ya ulinzi nje ya ukumbi wa Chuo cha Mipango inakokutana Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuchambua ripoti ya Escrow ilikuwa imeimarishwa, wakiwapo polisi wenye bunduki.
PAC Jumatatu wiki hii walikabidhiwa ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Ofisi ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali juu ya Escrow na  inatarajiwa kuiwasilisha bungeni Jumatano wiki ijayo.
Mwandishi wa NIPASHE mjini Dodoma alishuhudia polisi wenye silaha nje ya ukumbi huo, hali iliyoashiria kwamba watu wengine mbali na wajumbe wa kamati na waliokuwa wanaitwa kwa mahojiano hawakuhitajika kufika eneo hilo.
Hali ya ulinzi ikiwa ni ya kuogofya na baada ya kuzuiwa, waandishi walituma ujumbe kwa Zitto kupitia kwa mmoja wa maofisa wa Bunge, kwamba wamefika katika jengo hilo ili awaeleze yaliyokwishajiri na yanayoendelea kujiri.
Afisa huyo wa Bunge alipokea ujumbe huo na kuingia katika ukumbi wa jengo hilo ambako PAC inaendelea na kazi yake, baada ya dakika chache, alirudi na jibu alilodai kuwa linatoka kwa Zitto kwamba, amesema wako kazini na kwa hiyo hawezi kutoka kwa  ili kuzungumza na wanahabari. Hali hiyo iliwalazimisha wanahabari kuondoka eneo hilo.
Zitto alikuwa ameahidi kwamba angekutana na wanahabari jana kwa ajili ya kuwapatia taarifa kuhusiana na mchakato wa kuwahoji wahusika wa sakata la kuchotwa kwa zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka kwenye akaunti hiyo katika mazingira yenye utata.
Jumatatu wiki hii, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai aliikabidhi ripoti ya uchunguzi ya CAG kwa PAC kwa ajili ya kuipitia na kuwahoji watu kadhaa kabla ya kuwasilishwa bungeni na kujadiliwa na Wabunge.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment