
Wagonjwa wakiwa wamelazwa chini kwenye wodi ya Sewaaji, katika Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam jana. Picha na Anthony Siame
Pengine ni neno linaloweza kuwakilisha uhalisi wa hali ilivyo katika
baadhi ya hospitali kadhaa za Serikali nchini, ambako mamia ya wagonjwa
wanateseka kutokana na uhaba wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba ambao
umeendelea kuzikumba.
Wengi wa wagonjwa waliohojiwa wanalalamikia
kushindwa kumudu gharama za dawa ambazo wanapaswa kuzinunua kwenye
maduka wakisema hali hiyo inazifanya afya za Watanzania wengi wenye
kipato cha chini wanaozitegemea kuwa shakani.
Gazeti hili katika uchunguzi wake limebaini kuwa, uhaba huo pia umesababisha
hospitali nyingi kuwabana wagonjwa kwa kuwatoza
fedha kwa ajili ya huduma, ili kujijengea uwezo wa kununua dawa chache,
pamoja na vifaa tiba kwa ajili ya dharura.
Kwa jumla, hali ilivyo ni tofauti ya matarajio ya
wengi kwamba kungekuwa na mabadiliko, hasa baada ya Serikali kutangaza
kwamba imekwishalipa sehemu kubwa ya deni ililokuwa ikidaiwa na Bohari
Kuu ya Dawa (MSD).
Hivi karibuni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Dk Seif Rashid alisema wizara yake imeilipa MSD Sh20 bilioni ili
kupunguza makali ya uhaba wa dawa. MSD inaidai wizara hiyo zaidi ya
Sh90bilioni za ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Jana, Msemaji wa Wizara ya Afya, Nsachris Mwamwaja
alisema: “Siwezi kuzungumza chochote kwa sababu tayari waziri wangu
alishatoa tamko bungeni, kwa hiyo kauli yetu ndiyo hiyohiyo aliyotoa
mheshimiwa waziri.”
Sura halisi ya uhaba wa dawa inaonekana katika
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) na Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili ambako hali imeendelea kuwa mbaya kwani ukosefu huo wa dawa
umesababisha baadhi ya wagonjwa kuzidiwa na wengine kupoteza maisha kwa
kushindwa kumudu gharama za matibabu.
Hospitalini Ocean Road, mwandishi wetu alikutana
na mkazi wa Arusha, Ashura Iddi aliyefika kutibiwa na kufuatana naye
hadi katika duka alikokwenda kununua dawa alizoandikiwa.
Akisaidiwa na mwandishi huyo, Ashura ambaye
amekatwa mkono wake wa kushoto kutokana na saratani ya mkono iliyosambaa
hadi kifuani, aliambiwa na mfamasia katika Duka la Biomed lililo karibu
na ORCI kuwa dawa zake za mionzi zinagharimu Sh166,000.
Hata hivyo, mgonjwa huyo ambaye alikuwa akikohoa
mfululizo kiasi cha kutapika, hakuweza kununua dozi hiyo kwani hakuwa na
fedha hivyo kurudi wodini kuendelea kukaa akisubiri siku dawa
zitakapofika au kupata fedha.
Ashura amelazwa ORCI tangu Oktoba 27, mwaka huu na
anasema hajapata matibabu zaidi ya kupewa dawa za maumivu aina ya
diclofenac. “Nimekosa hata dawa ya allergy (mzio) ambayo inauzwa Sh1,000
nimeambiwa hakuna,” alisema Ashura.
Kaimu Mkurugenzi wa ORCI, Dk Diwani Msemo alisema bado hawajajua
iwapo fedha zilizotolewa na Serikali kupunguza makali ya uhaba wa dawa
zitasaidia kwa kuwa tatizo ni kubwa.
Mfamasia katika duka la dawa la Biomed, Hilal
Shamshudin alisema siku wagonjwa kati ya 20 hadi 50 hufika katika duka
hilo kununua dawa za mionzi.
Alisema hata baadhi ya madaktari nao hufika
kununua dawa hizo kwa ajili ya wagonjwa ambao pengine huwapa fedha
wawasaidie kuzitafuta.
Mfamasia huyo alisema dawa za mionzi ni ghali
kwani wapo wagonjwa wenye dozi kubwa ambao hutakiwa kununua dozi ambazo
gharama zake ni kati ya Sh3 na 4milioni.
Mwanamke mwingine, Saumu Mfyonsi ambaye alikuwa akisumbuliwa na saratani ya utumbo, alifariki jana kutokana na kukosa dawa.
Ndugu wa Saumu, Abdallah Mfyonsi alisema
waliandikiwa dawa za zaidi ya Sh2 milioni lakini wakati wakizitafuta
ndugu yao alifariki. “Wote huu ni umaskini,” alisema Mfyonsi huku
akibubujikwa na machozi.
Neema maduka ya dawa
Maduka mengi ya dawa yaliyojengwa pembezoni mwa
hospitali hizo za umma, yananeemeka kwa kupata wateja wengi ambao kila
wanapoandikiwa dawa na madaktari hulazimika kwenda kuzinunua nje ya
hospitali husika.
Katika maduka ya dawa yaliyopo mbele ya lango la
kuingilia katika Hospitali ya Manispaa ya Temeke, baadhi ya wafamasia
wake waliwaambia waandishi wetu kwamba dawa zinazoongoza kwa kuwa na
wateja ni zile zinazohusishwa na kina mama wajawazito na uzazi.
Katika orodha ya dawa zinazonunuliwa kwa wingi pia
zimo za kutibu malaria, shinikizo la damu na kisukari. “Hapa pia
tunauza kwa wingi, vifaa tiba kama mipira kwa wagonjwa waliofanyiwa
upasuaji (wa kupitishia mkojo) ambao hutumiwa na wanawake na wanaume,”
alisema mmoja wa wafamasia.
Waandishi walishuhudia mwanamume aliyeingia katika
duka hilo na kununua mpira wa mkojo wenye urefu wa mita 21, kwa ajili
ya mgonjwa wake aliyelazwa wodini.
Wakati hayo yakitokea, uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa kuna uhaba mkubwa wa dawa katika hospitali hiyo ya Temeke.
Chanzo chetu ndani ya hospitali hiyo kilisema hali
ya dawa ni mbaya na hakuna hata dawa za kutuliza maumivu, hivyo msaada
wa haraka unahitajika wakati wakiendelea kusubiri mgawo kutoka MSD.
Chanzo hicho kilieleza kwamba kwa sasa madaktari
wanalazimika kuwaandikia wagonjwa dawa ili waende kununua katika maduka
yaliyopo nje.
“Kwa sasa stoo yetu ya dawa haina kitu, kiasi
kidogo kilichopo kina dawa chache ambazo haziwezi kukidhi mahitaji ya
wagonjwa wanaofika hapa. Zaidi, tuna upungufu mkubwa wa vifaatiba muhimu
ambavyo pia wagonjwa wanalazimika kwenda kuvinunua nje ya hospitali,”
alisema ofisa mmoja ambaye aliomba jina lake lisitajwe.
Alisema dawa muhimu zinazohitajika kwa sasa ni
pamoja na amocyllin, ciprofloxcan, diclofenac, diclofenac injection,
cannular, misoprosol (kuzuia utokwaji wa damu kwa wajawazito),
multivitamin, albendazol na mobendazole.
Baadhi ya vifaa tiba muhimu vilivyopelea ni pamoja
na mipira ya kutolea mkojo kwa wagonjwa, (catheter), namba 16 na 18 ,
kifaa cha kuchomea sindano(cannular), mipira ya mikono na vitendanishi.
Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, hakuwepo hospitali jana na alipopigiwa simu, iliita bila majibu.
Muhimbili majanga
Katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Wodi za
Sewa Haji na Kibasila zimefurika wagonjwa hadi kwenye veranda na milango
ya wodi hizo kutokana na wagonjwa wanaotokana na ajali.
Msemaji wa Taasisi ya Mifupa ya Hospitali
Muhimbili (Moi), Almasy Jumaa alisema zaidi ya asilimia 60 wamepata
ajali za bodaboda na bajaji.
“Wodi hizo zina uwezo wa kulaza wagonjwa kwenye
vitanda 30 kila moja, lakini sasa idadi ya wagonjwa imekuwa ikiongezeka
hadi mara tatu ya uwezo wa wodi na sisi hatuwezi kukataa kuwapokea, kwa
hiyo pamoja na matatizo mengine, tunawapokea na kuwalaza ndiyo maana
unaona wamejaa kiasi hicho,” alisema Almasy.
Mmoja wa wagonjwa, Elizabeth Biligimana alisema tangu amelazwa
na mgonjwa wake katika hospitali hiyo, Aprili mwaka huu kwa ajili ya
uchunguzi wa tumbo kujaa, hajawahi kupata dawa za bure.
“Mara nyingi naambiwa ninunue baadhi na baadhi
napata huko ndani, ukiniuliza kuhusu kununua dawa naona kama unatonesha
vidonda vyangu,” alisema Biligimana.
Almasy alisema japokuwa hawezi kuelezea kwa kina
tatizo lililopo, lakini uhaba wa dawa umekuwa kikwazo cha utoaji wa
huduma katika viwango vinavyotakiwa kwa kuwa wagonjwa wanalazimika
kuandikiwa kutafuta dawa nje ya hospitali.
“Kwa kiasi fulani utaratibu wa uchangiaji ambao
wagonjwa wanatakiwa kuchangia huduma ndiyo ambao umekuwa ukitusaidia
angalau kupata fedha kidogo kwa ajili ya kupata dawa za kusaidia
kunusuru hali,” alisema.
Hata hivyo, kuhusu kiwango cha uhaba na hatua
zinazochukuliwa, alisema hawezi kulizungumzia hilo kwa kuwa tayari
Waziri wa Afya alishatoa tamko na kueleza kwamba Serikali imeshatoa
fedha kwa MSD kwa ajili ya kulipa madeni yake na kusambaza dawa katika
hospitali zote za Serikali.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment