Pages

Monday, November 24, 2014

DK. GHALIB BILAL AWAHIMIZA WAHITIMU WAWE WABUNIFU

Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Bilal (pichani), amewataka wahitimu wa Chuo Kikuu cha Uongozi cha Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ESAMI) kuwa wabunifu wa kutatua changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu wa sasa.
Bilal alitoa wito huo mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Arusha wakati alipowatunuku vyeti wahitimu zaidi ya 500 wa ngazi mbalimbali za uongozi kutoka Bara la Afrika.
“Pamoja mmehitimu leo, siyo mwisho wa elimu sasa mnatakiwa kubuni vitu vipya ili kusaidia jamii kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kila kukicha,” alisema.
Alisema ili mwanafunzi awe bora siku zote ni lazima awe mbunifu ili kuendana na mabadiliko yanayotokea ulimwenguni kila kukicha.
Alisema kwa  sasa duniani kuna ushindani wa aina mbalimbali, hivyo bila kuwa wabunifu itakuwa kazi bure hata kupata kazi.
“Nawaomba tu hasa vijana mliohitimu hapa leo ongezeni kuwa wabunifu ili msaidie jamii inayotuzunguka katika nchi zetu,” alisisitiza.
Pia alikipongeza chuo hicho kwa kutoa wahitimu wenye sifa nzuri ya kuchapa kazi kila wanakokwenda ulimwenguni kote na kuwataka waendelee kutoa elimu bora bila kuchoka.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo ambaye kwa sasa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, akiwa mmoja wa wahitimu wa mahafali hayo, alishukuru Mungu kuhitimu masomo yake na kutumia fursa hiyo kuwaaga waandishi wa habari.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment