
Mkurugenzi wa SSRA, Irene Isaka
Hali hiyo inaweza kukwamisha mifuko hiyo kuwalipa mafao wanachama
wake, kujiendesha yenyewe na kuwekeza katika miradi mbali mbali.
Deni hilo linatokana na serikali na taasisi zake kukopa kwenye mifuko hiyo na kutopeleka michango ya wanachama.
Mkurugenzi wa SSRA, Irene Isaka, alisema deni hilo ni pamoja na
lililotokana na ahadi ya serikali kulipa malipo ya pensheni kwa
wafanyakazi ambao walikuwa hawachangii kwenye Mfuko kabla ya 1999.
Isaka aliyekuwa akizungumza katika mkutano ulioitishwa na Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na kuwakutanisha
wakurugenzi wa kifumo ya hifadhi ya jamii, Wizara ya Fedha, Ofisi ya
Mdhibiti na Mkaguzi wa Mkuu wa Hesabu za Serikali, SSRA na Gavana wa
Benki Kuu ya Tanzania (BoT), alisema deni jingine ni dhima ya mifuko
ambayo ni kifurushi cha ahadi ambacho mwanachama ameahidiwa hadi siku
anafariki na kwamba mifuko isipokuwa na hazina ya kutosha inabadilika
kuwa kuwa deni.
Isaka alisema iwapo serikali itaendelea kukopa na kutopeleka
michango ya wanachama wake, mifuko hiyo itaathirika kiasi cha kushindwa
kulipa mafao kwa wanachama wake.
”Athari tuliyonayo, mifuko yetu ni ya pensheni, hasara ni ya
mifuko. Mwanachama hatamsamehe mwenye mfuko kwa kushindwa kumlipia,
kadri deni linavyoongezeka ndivyo Mfuko unaumia na baadaye kushindwa
kulipa mafao yanayotakiwa,” alifafanua Isaka.
Alisema kwa madeni hayo Mfuko ambao unanunua kifurushi cha ahadi
kwa mwanachama na unatakiwa kutimiza anapostaafu, utaendelea kuharibika
kadri muda unavyozidi iwapo utashindwa kulipa madeni.
Awali, Kaimu CAG, Athumani Selemani, akizungumza alisema zaidi ya
Sh. Trilioni 1. 37 ni deni la serikali na taasisi zake walikopa kutoka
kwenye mifuko hiyo kwa shughuli mbalimbali.
Alisema zaidi ya Sh. trilioni 7.9 ni deni la PSPF la kuanzia 1999
ikiwa ni fedha za kuwalipa mafao wanachama ambao walikuwa hawachangii
kwenye Mfuko lakini kwa mujibu wa sheria walioaswa kulipwa.
Selemani alibainisha deni hilo kwa kila mfuko inavyoonekana kwenye
mabano ni PPF ( bilioni 192), NHIF ( bilioni 107), NSSF ( bilioni 467),
PSPF ( bilioni 4.29), LAPF ( bilioni 170) na GEPF (bilioni 6.86).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile,
alithibitisha serikali kulitambua deni hilo na kwamba ni lazima ilipe
ikiwa ni pamoja na deni ya PSPF kabla ya mwaka 1999.
Pamoja ka kukiri na kuahidi kulilipa madeni hayo, Dk. Likwelile
hakueleza ni lini serikali italipa wala utaratibu utakaotumika
kuyapunguza.
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuanza kikao hicho,
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alisema waliwaita BoT, Katibu Mkuu
Wizara ya Fedha, CAG, SSRA, Wenyeviti wa bodi na Wakurugenzi wa mifuko
ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya kulijadili suala hilo.
Alisema lengo ni kujadili namna ya serikali kulipa deni hilo ili
kuiwezesha mifuko hiyo kusonga mbele kwa kulipa mafao wanachama wake na
kuwekeza.
Kabwe alisema serikali zote duniani zinakopa kwenye mifuko hiyo,
lakini tatizo kubwa kwa serikali ya Tanzania ni kutolipa, jambo ambalo
alisema ni hatari kwa uendeshaji endelevu wa mifuko hiyo.
”Tuna tatizo la serikali kukopa kwenye mifuko kwa ajili ya miradi
mbalimbali na kutolipa, ni kawaida kwa nchi nyingine duniani kukopa na
kurudisha tofauti kwa serikali ya Tanzania hairudishi,” alisema Kabwe.
Aliyataja baadhi ya madeni kuwa ni fedha za ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma Sh. milioni 800 na deni la PSPF la kabla ya 1999.
Alisema hali hiyo ikiachwa kuwa kama ilivyo sasa mifuko itashindwa
kuwekeza katika miradi mbalimbali, hivyo ni muhimu madeni yalipwe ili
mifuko iendelee kulipa madeni na kwamba itafika wakati itauza samani
zake na kushindwa kufanyakazi.
Deni hilo ni takribani nusu ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15 ambayo ni Sh. trilioni 19.8.
Wakati serikali ikidaiwa na mifuko hiyo, kiasi hicho cha fedha,
Deni la taifa hadi Machi mwaka huu, lilifikia Shilingi trilioni 30
ikilinganishwa na Shilingi trilioni 23.6 Machi mwaka uliopita 2013.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment