
Akizungumza katika mahojiano maalum na NIPASHE nyumbani kwake
Donge, visiwani Zanzibar, Ameir ambaye aliwahi pia kuwa Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi na Waziri wa Habari, alisema Mkapa alikuwa na sifa
zilizoianishwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 1995, anazoamini kwamba bado
zinahitajika katika uchaguzi ujao na zaidi ya hayo, vilevile (Mkapa)
alikuwa ni makini, mchapakazi na asiye na ubinafsi.
Ameir alizitaja baadhi ya sifa zilizoainishwa na CCM wakati Mkapa
alipopata nafasi ya kugombea na mwishowe kuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kuwa ni, elimu ya chuo kikuu, uwezo wa kuongoza na
uzoefu wa kutosha.
“Tena sifa hizo za Chama Cha Mapinduzi zilipowekwa na mimi
nilikuwapo… kwa hiyo sipingani nazo. Bado naona zinafaa,” alisema Ameir,
akiongeza kuwa ni sifa hizo, ikiwamo ya elimu ya chuo kikuu, ndizo
zilizochangia kumuondoa Augustine Mrema aliyeihama CCM na kujiunga na
chama kikuu cha upinzani wakati huo cha NCCR-Mageuzi. Hivi sasa Mrema ni
Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP).
Ameir alimsifu Mkapa, akisema anamfahamu vizuri rais huyo wa awamu
ya tatu kwa vile alifanya naye kazi wakati walipokuwa waandishi wa
habari na baadaye kuteuliwa naye kuwa waziri katika serikali yake.
“Unajua Mzee Mkapa ni mtu makini, mtu ambaye hapendi majungu. Usije
ukampelekea jungu. Na mimi nimegundua toka tuko gazeti la Uhuru. Kama
hujamzoea utamuona kama mtu anayeringa hivi… lakini nimemgundua mtu
yeyote anaweza kumwingia,” alisema.
“Ni msomi, ni very serious person, principled (ni mtu makini,
mwenye kufuata kanuni) na ni mzalendo. Ni kiongozi makini na kama
utamuelewa, atakuwa rafiki yako mkubwa,” alisema Ameir.
UMRI WA URAIS
Kuhusu umri wa urais, Ameir alipendekeza uanzie miaka 40 kwani ana
amini kuwa huo ndiyo umri mzuri zaidi kwa sababu akili (ya mtu) tayari
inakuwa imekomaa na anajua kuwa amepewa dhamana ya kulitumikia taifa.
Alisema rais ni mtu mkubwa kwa kuwa ndiye mkuu wa nchi na Amiri
Jeshi Mkuu na hivyo kama (rais) bado ana mambo ya ujana, ni hatari kwa
nchi.
“Mimi vijana watanisamehe… wanaweza kunishangaa kwamba hili dingi
ni conservative (huyu mzee ni mhafidhina). Lakini miaka 40 ni umri
mzuri,” alisema na kuongeza:
“Siyo lengo langu kuwazuia vijana kuwa marais. Lakini lengo langu
ni (kuona) kuwa rais akiwa na umri angalau miaka 40, huwa hababaishwi
kwa sababu ujana una mambo yake. Mtanisamehe vijana.”
“Rais ni mtu mkubwa sana. Ndiye Amiri Jeshi Mkuu, watu wote, hata
mkuu wa majeshi anampigia saluti. Mkipata mtu ambaye hajatulia vizuri,
mnaweza kupata matatizo.”
Alitolea mfano kwa Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC), akisema alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza, alikuwa
kijana mdogo lakini aliweza kuongoza kwa kuwa alipendekezwa na
kusimamiwa na jeshi na kwamba kwa sasa amekomaa na hivyo amekuwa rais
mtendaji.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment