Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
Ofisi Ndogo ya Bunge jijini Dar es Salaam, imewataka
wabunge wote wateule walioko majimboni kufika katika ofisi hizo
Jumatano wiki hii kwa ajili ya kushiriki hafla ya kuapishwa kwa Rais
Mteule itakayofanyika Novemba 5, mwaka huu katika Uwanja wa Uhuru.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu
Katibu wa Bunge, John Joel, alisema wabunge wateule watakaohudhuria
hafla hiyo wanatakiwa kuja na vyeti vya kuteuliwa walivyopewa na
Wasimamizi wa Uchaguzi.
“Kila Mbunge mtarajiwa, atatakiwa kuwasilisha cheti kwa Maofisa wa
Bunge wakati wa mchakato wa usajili na kitambulisho kingine chochote
kinachotolewa na mamlaka inayotambulika na kinachomtambulisha jina lake
kamili kama linavyoonekana kwenye cheti cha uteuzi wa ubunge,”
alisisitiza.
Aidha, alisema mchakato wa usajili wa wabunge wateule utafanyika
katika viwanja vya Bunge la 11 na kuongeza wabunge hao watajitegemea
usafiri wa kuelekea bungeni.
Joel alisema mkutano huo utaanza siku ambayo Rais Mteule atakapoitisha Bunge.
Alisema siku hiyo shughuli mbalimbali zitafanyika zikiwamo za
uchaguzi na kiapo kwa Spika, viapo vya wabunge, uthibitisho wa jina la
Waziri Mkuu, uchaguzi wa Naibu Spika na ufunguzi rasmi wa Bunge la 11.
Alivikumbusha vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu vinavyotaka
kusimamisha mgombea wa nafasi ya Spika vianze mchakato wa kupata
mgombea katika ngazi ya vyama baada ya tangazo kutolewa na kuwasilisha
jina lake kwa Katibu wa Bunge.
Alivisistiza vyama kuzingatia kuwa mgombea wa nafasi hiyo anaweza
kuwa mbunge au mwanachama yeyote wa chama hicho kwa masharti kwamba siyo
mbunge mteule.
Hali kadhalika, alisema vyama vya siasa vinatakiwa kuwasilisha jina
la mgombea Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) siku tano kabla ya uchaguzi
kujiridhisha kwamba mgombea ana sifa za kuwa mbunge.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment