Rais Buhari akishangilia baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa
Nigeria, hivyo kupata nafasi ya kuliongoza tena taifa hilo la Afrika
Magharibi.
Miaka ile ya
1980 nilikuwa nasoma sana magazeti ya kimataifa kama ‘Africa,’ ‘Africa
Now,’ ‘Africa Events’ na mengineyo yaliyoruhusiwa kuingia nchini. Haikuwepo mitandao ya kijamii kama ilivyo leo wala mawasiliano ya kompyuta, hivyo tulipata habari nyingi za kimataifa
kupitia magazeti ya kimataifa.
Ni katika magazeti hayo, nilisoma habari za
mwanajeshi mwenye cheo cha Meja Jenerali, Muhammadu Buhari aliyeingia
madarakani nchini Nigeria kwa mapinduzi Desemba 31, 1983. Miaka miwili
ya utawala wake ilikuwa michungu kwa wafanyakazi, madereva na wakorofi.
Siku chache baada ya kuweka mambo sawa yaani
kuunda Baraza la Kijeshi, ‘mjeshi’ huyo alifanya ziara kwenye kampuni
moja ya umma (nadhani ya mafuta), ambapo yeye na msafara wake walifika
mapema kabla ya baadhi ya wafanyakazi na wakurugenzi.
Hakuwaacha hivi hivi, aliamuru wanajeshi kuwachapa viboko wote waliochelewa kufika.
Buhari aliruhusu wanajeshi kwenda barabarani
kufanya kazi ya Askari wa Usalama Barabarani. Tofauti yao ni kwamba wao,
hawakuwa wanasimama kuruhusu magari kupita bali walikuwa wanawafuata
madereva wanaokiuka sheria na kuwacharaza bakora sawasawa. Halafu
aliwatawanya askari kwenye ofisi za umma ambako wafanyakazi
waliojijengea utamaduni wa kuchelewa kazi walikula bakora.
Huyo ni Muhammadu Buhari wa wakati ule.
Niliposikia ametangazwa mshindi wa kiti cha urais, katika uchaguzi mkuu
wa kidemokrasia Nigeria hivi karibuni, haraka nilikumbuka bakora kwa
madereva, kurushwa kichura kwa maofisa kama adhabu kwa kuchelewa kwao na
kuamuru kunyongwa wauzaji ‘unga’ na kulazimisha usafi kwa kuwatia jela
vikojozi wa barabarani.
Ingawa kuna watu walifurahia alivyosimamia
nidhamu, wanajeshi wenzake walimpindua mwaka 1985 na akazuiwa nyumbani
kwake. Najiuliza, mjeshi huyu hatapenda kuchota mambo ya zamani na
kuyatumia sasa akiwa rais wa kuchaguliwa?
Wampenda, wamgeuka
Siku za mwanzo za utawala wake, wananchi
walimfurahia Buhari aliyetarajiwa kuondoa matatizo makubwa ya kiuchumi
yaliyokithiri wakati wa utawala wa kiraia wa Shehu Shagari, lakini hatua
kali alizochukua kukomesha uzembe, kufukuza wahamiaji, kucharaza viboko
maofisa, alikasirisha wengi.
Ilionekana wananchi walihitaji mabadiliko makubwa
ili kuondoa dhuluma, ufisadi, uzembe, utovu wa nidhamu uliokithiri enzi
za Shehu Shagari, lakini alipoanzisha kampeni iliyoitwa “Vita Komesha
Utovu wa Nidhamu” ambayo iliwagusa wanasiasa na wafanyabiashara wengi,
wakashitakiwa kwa rushwa kwa lengo la kuipa heshima Nigeria, alichukiwa.
Utawala wake ulizuia uhuru wa habari, vyama vya
siasa na vyama vya wafanyakazi. Hivyo, alipopinduliwa Agosti 27, 1985 na
‘mjeshi’ mwingine Meja Jenerali Ibrahim Babangida, wengi walipokea
habari hizo kwa shangwe. Baada ya kupinduliwa alizuiliwa nyumbani kwake
katika mji wa Benin hadi mwaka 1988.
Changamoto
Buhari hakupotea kwenye siasa, alianza kufuata nyayo za
mwanajeshi mwingine Olusegun Obasanjo, ambaye baada ya kutawala kijeshi
kuanzia Februari 13, 1976 hadi Oktoba 1, 1979 alirejea kutawala kama
raia kuanzia Mei 29, 1999 hadi Mei 2007. Hali hiyo ilimvutia Buhari,
akawania urais kama raia mwaka 2003 lakini aliangushwa na Obasanjo wa
chama cha People’s Democratic Party (PDP).
Matokeo yalimpa hamasa ya kugombea tena mwaka 2007
na aliangushwa na mgombea wa PDP, Umaru Yar’Adua katika uchaguzi ambao
mchakato wake ulishutumiwa na waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa kwamba
ulitawaliwa na ukiukwaji wa taratibu. Hakukata tamaa, alijitosa kwa
mara ya tatu, mwaka 2011 pia alipigwa mwereka na Goodluck Jonathan wa
PDP.
Udhaifu alioonyesha Jonathan katika kupambana na
rushwa na zaidi vita dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram, ulitumiwa
na Buhari kama mtaji wa kisiasa. Mwaka 2014 aliteuliwa na Chama cha All
Progressives Congress (APC) kuwa mgombea urais uliopangwa Machi 28,
2015. Vitu vilivyomwongezea mtaji na mvuto kwa wapigakura ni heshima
aliyojijengea kwamba si fisadi, kwamba kati ya madikteta waliotawala
Nigeria, yeye hakuwahi kufuja fedha za umma.
Aliwahi kuwa mkuu wa nchi akiwa na magwanda na kwa sasa wanaamini kuwa ataweza kupambana na Boko Haram.
Japokuwa kulikuwa na wagombea wengine 14 wa urais,
ushindani ulikuwa kati ya Buhari na Jonathan wa PDP. Jonathan
aliangushwa na Buhari kwa tofauti ya kura milioni 2.5. Kwa anguko hilo,
Jonathan amekuwa rais wa kwanza kushindwa katika uchaguzi na kukabidhi
madaraka kwa amani.
Changamoto
Buhari amerithi mikoba ya Jonathan huku nchi ikiwa
inakabiliwa na changamoto kadhaa na kubwa zaidi ni usalama (kupambana
na Boko Haram), kushuka bei ya mafuta (asilimian 70 ya mapato ya
Serikali yanatokana na mafuta), na kushuka thamani ya naira (fedha za
Nigeria).
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment