Social Icons

Pages

Thursday, April 09, 2015

VIGOGO RUBADA WASIMAMISHWA KWA UFISADI

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, amewasimamisha kazi wakurugenzi watatu wa Mamlaka ya Ustawishaji wa Bonde la Mto Rufiji (Rubada) kwa tuhuma za ufisadi wa zaidi ya Sh. bilioni mbili.
Wasira alitangaza uamuzi huo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam. Aliwataja waliosimamishwa kazi rasmi kuanzia jana kuwa ni Kaimu Mkurugenzi wa Rubada, Aloyce Masanja; Mkurugenzi wa Fedha, Filozi Mayayi na Mkurugenzi wa Mipango na Utawala, Tabu Ndatulu.
Alisema kusimamishwa kazi kwa vigogo hao kunafuatia kamati iliyoundwa na wizara hiyo chini ya Mwenyekiti wake ambaye ni  Kaimu Mkurugenzi wa Mkaguzi wa Serikali, Semloki Mwanjika, kuchunguza tuhuma na malalamiko mbalimbali yaliyokuwa yanatolewa na wawekezaji kuhusu Rubada, kufanya kazi kwa zaidi ya miezi mitano na kubaini ubadhirifu huo.
“Kwa mamlaka niliyonayo mimi, nawasimamisha kazi rasmi kuanzia leo, kwa hatua nyingine za makosa ya ubadhirifu wa fedha na rushwa nitaliachia Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wafanye kazi yao baada ya mimi kukamilisha kazi ya kuwawajibisha kwa kosa na ukosefu wa nidhamu kazini, ripoti zote nitaziwasilisha Polisi na Takukuru,” alisema Wasira. Alisema hatua nyingine zitachukuliwa dhidi ya vigogo hao baada ya Polisi na Takukuru kukamilisha uchunguzi dhidi yao kuhusiana na tuhuma hizo.
Alisema wawekezaji walitoa Sh. bilioni 2.7 kwa ajili ya kuwekeza kwenye miradi mbalimbali ya kilimo,  Sh. milioni 714 zitumika kwa kazi hiyo na Sh. bilioni 2.3 matumizi yake hayajulikani. Wasira alisema Sh. milioni 329 zilizotengwa kwa mradi wa ujenzi wa bonde la mto Rufiji nazo hazijulikani zilipo na nyingine Sh. milioni 58 ambazo wafanyakazi walikatwa kuchangia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwenye Shirika la NSSF  hadi sasa hazijapelekwa.
Alisema katika kipindi chote kulikuwa na malalamiko ya utendaji mbovu wa viongozi hao na baada ya tume kufanya uchunguzi wake kuanzia Novemba mwaka jana, ilibaini walikuwa ni wabadhirifu wa fedha, ubinafsi na wala rushwa. “Kwanza wamejitengenezea mfumo mbaya wa kujinufaisha wenyewe na usiokuwa na mgawanyo wa majukumu kwa watendaji wote hali inayosababisha ulegevu kwenye kuwajibika na kusababisha hadi maofisa wanasafiri na fedha mifukoni,” alisema Wasira.
Alifafanua kwa mujibu wa uchunguzi wa kamati hiyo, kiasi cha Sh. milioni 13 zilitumika kwa matumizi binafsi na Sh. milioni 13 vigogo hao kujikopesha wenyewe. Wasira, alisema pia kamati hiyo ilibaini kuwa licha ya matumizi mabaya ya fedha pia mamlaka hiyo ilikuwa haifuatilii malipo ya kampuni binafsi ambazo zinafanyakazi na Rubada.
Kuhusu wawekezaji ambao walitoa fedha zao kuwekeza, lakini hawakupewa maeneo ya uwekezaji, alisema wanaidai serikali fedha hizo au wapewe ardhi kwaajili ya uwekezaji. Wasira alitaja mapendekezo mengi yaliyotolewa baada ya kupokea ripoti ya kamati hiyo kuwa ni bodi itafute mtu mwenye sifa ya kukaimu nafasi ya Kaimu Mkurugenzi wa Rubada. Mengine ni bodi ianze mara moja mchakato wa kutafuta viongozi watakaosimamia nafasi hizo baada ya wakurugenzi hao kusimamishwa.
“Wakati haya yote yakiendelea, taratibu rasmi za utumishi wa umma za kuwasimamisha kazi na utaratibu wa kushughulikia tatizo zinaendelea,” alisema Wasira. Kuhusu uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji, Wasira alisema suala hilo analifahamu Rais Kikwete na analifanyia kazi.
 
KAULI YA MASANJA
Masanja, alipoulizwa na NIPASHE kuhusu hatua ya Waziri Wasira kumsimamisha kazi na wenzake kwa tuhuma za ufisadi, alidai kuwa yeye siyo mfanyakazi wa Rubada tangu Septemba mwaka jana baada ya kuacha kazi kutokana na sababu zake binafsi.
Alisema aliandika barua ya kuomba kuacha kazi kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na kupewa baraka zote. Tangu Masanja ateuliwe na bodi ya mamlaka hiyo kukaimu ukurugenzi wa Rubada ni takribani miaka mitatu kutoka kwa  aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo.
Tangu wakati huo, Rais Jakaya Kikwete alikuwa hajateua Mkurugenzi wa Rubada, hivyo Masanja kukaimu nafasi hiyo kutoka kwa bosi wake huyo. Rubada ilianzishwa mwaka 1970 kwa lengo la kuendeleza bonde la  Mto Rufiji na Pwani, Morogoro, Iringa, Njombe, Ruvuma, Mbeya na sehemu ya Lindi.
Mbali na kuendeleza maeneo hayo, pia Rubada iliundwa kwa lengo la kutangaza vivutio na uwekezaji kwenye sekta ya kilimo nchini.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: