
Kamishna wa Maadili, Jaji mstaafu, Salome Kaganda,
amesema moja ya mambo ambayo walikabiliana nayo wakati wa sakata la
akaunti ya Tegeta Escrow, ni kwa wanasiasa kujitetea kwamba kitendo
cha kuomba fedha kwao ni jambo la kawaida, kwani kufanya hivyo wanakiuka
maadili ya utumishi wa umma.
Jaji Kaganda alitoa kauli hiyo katika warsha ya wadau ya kujadili
rasimu ya mwongozo wa maadili wa viongozi wa umma, iliyofanyika jana
jijini Dar es Salaam. Warsha hiyo iliwashirikisha viongozi na watumishi wa umma, wawakilishi wa asasi za kiraia na wanasiasa.
Akifafanua, Jaji Kaganda alisema tabia ya ukosefu wa maadili ya
umma imekuwa ikijirudiarudia katika maeneo mengi yakiwamo matumizi
mabaya ya madaraka, vitendo vya rushwa, kuomba, kushawishi na kupata
fedha katika mazingira yasiyo halali, jambo ambalo liliwapa shida
wakati wakishughulikia wahusika wa sakata la Escrow kutokana na
wanasiasa wakati wanahojiwa kusema kuwa kwao kuomba fedha ni jambo la
kawaida.
“Mwongozo huu pia umetaja vitendo vya ukiukwaji wa maadili ya
viongozi wa umma…matumizim mabaya ya madaraka, taarifa za serikali,
vitendo vya rushwa, mgongano wa maslahi, kushindwa kutoa tamko la
rasilimali na madeni, unyanyasaji wa kijinsia, kuomba, kupokea,
kushawishi na kujipatia maslahi ya kifedha yasiyostahili..katika hili
tulipata shida sana wakati wa suala la Escrow…wanasiaasa wakisema kwao
kuomba fedha ni jambo la kawaida,” alisema jaji Kaganda.
Baadhi ya wanasiasa waliohusika na kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya
Shilingi bilioni 300 kutoka katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa
Benki Kuu (BoT) na kuhojiwa na sekretarieti hiyo ni pamoja na aliyekuwa
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka;
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na Mbunge wa Sengerema,
William Ngeleja.
Hata hivyo, Chenge alikataa kuhojiwa na kuweka pingamizi mahakamani. Kufuatia sakata hilo, Ngeleja, aliondolewa katika nafasi ya
uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala huku
Chenge akiondolewa uenyekiti wa Kamati ya Bajeti.
Kadhalika, Profesa Tibaijuka, Chenge na Ngeleja walisimamishwa
ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment