Social Icons

Pages

Friday, March 13, 2015

VIFO AJALI YA BASI VYAFIKIA 50

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza
Idadi ya watu waliopoteza maisha kwenye ajali ya basi iliyotokea juzi eneo la Changarawe, Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, imeongezeka kutoka 42 na kufikia 50.Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, alisema taarifa za hospitali zinaonyesha kuwa watu wengine wanane wamefariki dunia kutokana na ajali hiyo. Alisema tayari miili 17 ya marehemu waliokuwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa, imetambuliwa na kati ya hiyo, 14 imechukuliwa na kwamba marehemu 10 bado haijatambulika.
Masenza alisema marehemu 21 wametambuliwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mafinga, nane kati yao wamechukuliwa na wawili hawajatambulika. Alisema basi hilo likitokea mkoani Mbeya lilikuwa na watu 49 ambao ni abiria 47 na dereva na kondakta, lakini njiani walipakiza watu wengine ambao hawakuingizwa kwenye orodha na ndiyo maana taarifa zinakanganya.
“Wakati wanaandika watu kwenye rejista ya wasafiri, jumla walikuwa 47 lakini wanaopandia njiani hawaandikwi na hili ni tatizo kubwa,” alisema. Masenza aliongeza: "Hii imetokana na kupiga hesabu ya miili iliyochukuliwa, majeruhi waliopo hospitali na majeruhi walioruhusiwa na kukuta kwamba basi hilo lilikuwa limebeba watu wengi kupita maelezo.”
Akizungumzia suala la barabara, Masenza alikiri kwamba  kulikuwa na mwendo kasi, ufinyu wa barabara na mteremko mkali kwenye eneo la tukio. Alisema kasoro nyingine ni barabara hiyo kutokuwa na alama za barabarani, lakini kwa sehemu ya barabara kuna mashimo makubwa ambayo yaliyosababisha ajali.
“Kwa kuwa barabarani kulikuwa na mashimo kila moja ya magari hayo yalikuwa yakijaribu kukwepa mashimo na ndipo kontena lilipoliangukia basi,” alisema. Hata hivyo, aliwataka wanaosafirisha makontena kuyafunga vizuri ili kuepuka ajali kama hiyo.
Kuhusu mashimo barabarani, Masenza alisema uhaba wa fedha umeuchelewesha Mkoa kuyaziba licha ya kwamba kuna mdau alitoa kokoto kwa ajili ya kuyafukia. “Barabara hiyo imetengenezwa muda mrefu na sasa inahitajika kufumuliwa na kujengwa upya, lakini hatutaweza kufanya hivyo kutokana na uhaba wa fedha,” alisema.
 
MAJERUHI WASIMULIA
Akizungumza na NIPASHE, mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, Dominick Shauri, alisema hali yake inaendelea vizuri japo amepata majeraha kichwani na sehemu mbalimbali za mwili wake. Shauri alisema wakati wa ajali hiyo, ghafla alisikia sauti ya watu waliokuwa wamekaa viti vya mbele wakitoa sauti Mungu wangu, lakini hakujua kilichotokea kwa sababu alikuwa amekaa viti vya nyuma.
“Nilishitushwa sana kuona watu wanataja jina la Mungu, lakini mimi binafsi sikujua kilichotokea,baadaye niliona viti vilivyokuwa mbele yangu vimesogea nyuma na ghafla nikaona kimya nami pia nikashikwa na butwaa, sikujua kilichoendelea,” alisema.
Alisema baadaye alijikuta yupo Hospitali ya Wilaya ya Mufindi na hakujua amefikaje hospitali. “Nikiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, nilisikia baadhi ya watu waliofika hospitalini hapo na wauguzi wakisema kuwa kuna gari ya Majinja imepata ajali, ndipo nilipogundua na mimi ni miongoni mwa waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo,” alisema Shauri.
Naye Martin Haule, alisema: “Kiukweli ni mwendo kasi wa basi walilokuwa wakisafiria lakini mbele niliona kuna lori kubwa la mizigo ambalo linakuja kwa kasi sana sikujua kilichoendelea, baadaye nikajikuta nipo Hospitali ya Mufindi ninapatiwa matibabu.”

MGANGA MFAWIDHI
Mganga Mkuu Mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Dk. Robert Salim, alisema juzi hospitali yake ilipokea majeruhi tisa kutoka hospitali ya Wilaya ya Mufindi na mmoja wao alifariki dunia. Alisema wengine wanne hali zao ni mbaya na wanne wanaendelea vizuri.
Alisema kwa sasa wanatarajia kuwapeleka majeruhi wawili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi kutokana na kuwa hali zao ni mbaya. Pia aliwataja majeruhi waliopo hospitalini na hapo kuwa ni Dominick Shauri, Fadhili Kalenga, Elius Mwakapale na Nehemia Mbugi.
Wengine ni Mustafa Ramadhani, Tito Kyando, Mamba Impyana na Martin Haule. Aliyefariki dunia kukamilisha idadi ya majeruhi tisa alimtaja kuwa ni Osward Mwinuka (54). Hadi jana jioni, shughuli ya kutambua miili ya marehemu ilikuwa ikiendelea katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa na ya Wilaya ya Mufindi ya Mafinga na baadhi ya miili ya marehemu ilichukuliwa na ndugu zao kwa maziko.
 
MBATIA AKOSOA
Wakati huo huo, Mbunge wa Kuteuliwa na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR- Mageuzi, James Mbatia, ameitaka serikali kutoa taarifa rasmi juu ya tukio hilo ili wale wote watakaobainika kuwa ni chanzo wachukuliwe hatua kali ikiwamo kufikishwa mahakamani mara moja.
Alisema Watanzania hawawezi kuendelea kuvumilia kuona damu za wenzao zinamwagika huku wahusika ambao kwa namna moja ama nyingine, ni sababu ya ajali hizo. Alisema upo uzembe wa makusudi unaosababisha ajali hizo ambao unasababishwa na baadhi ya watendaji kushindwa kutumia fedha vizuri zinazotolewa kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ambao kwa namna moja ama nyingine ni sababu mojawapo ya ajali hizo.
“Inauma sana jamani, damu za Watanzania zinaendelea kumwagika kwa ajali huku Watanzania tunajidanganya kwamba ni mipango ya Mungu, ajali hizi si mpango wa Mungu bali ni za kutengenezwa, ajali ile imetokea katika eneo lenye shimo, yenye ubovu wa barabara halafu tunasema ni mpango wa Mungu,” alisema Mbatia na kuongeza:
“Ninaitaka serikali itoe taarifa rasmi haraka iwezekanavyo na kama ikigundulika mtu yeyote alizembea ama kwa kushindwa kutimiza wajibu wake katika kila ngazi, wachukuliwe hatua ikiwamo kufikishwa mahakamani. Lazima watu wawajibike katika hili.”
Mbatia alisema ipo haja kwa serikali kuangalia upya mifumo yake kwa madereva wanaobainika kukiuka sheria za barabarani na kunyang'anywa leseni zao. Pia lisema anatarajia kulipeleka suala hilo bungeni ili madereva wote wawe wanasoma miezi sita kufahamu umuhimu wa kuzingatia sheria za barabarani na athari zake. Lingine alilosema anatarajia kulipeleka bungeni ni kuhusu magari ya mizigo (malori), kupigwa marufuku kutumia barabara zinazotumiwa na magari ya abiria.
 
CUF YATOA POLE
Chama cha Wananchi (CUF), kimetuma salamu za pole na rambirambi kwa majeruhi wote wa hiyo. “Tukio hili ni baya sana na la kusikitisha kwa Watanzania. Si rahisi kuelezea tukio hili bila kulengwa ama kutokwa na machozi,” ilieleza taarifa ya CUF jana.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Shaweji Mkweto, ilieleza kuwa matukio ya namna hiyo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara na hakuna hatua za mashiko za kumaliza tatizo hili. “Kwa ajali hii licha ya uzembe waliofanya madereva, lakini miundombinu ya eneo ya ajali haikuwa sawa kutokana na mashimo yaliyopo. Barabara nyingi za lami Tanzania zimeharibika sana na marekebisho yake hayafanyiki na kama yakifanyika, ni kidogo ama kiubabaishaji,” alisema na kuongeza:
“CUF Tunaitaka serikali kupitia upya mfumo wake wa marekebisho ya barabara ili kuhakikisha ubovu wake hauchangii kabisa katika kuleta ajali barabarani. Japo hii si tiba ya ajali za barabarani, lakini kwa kiasi fulani itapunguza.”
Juzi, ajali mbaya ilitokea katika mji wa Mafinga, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa baada ya basi la kampuni ya Majinja Express lenye namba za usajili T 438 CDE, kugongana uso kwa uso na lori la mizigo  na tela namba T 698 APJ na kisha kontena lililokuwa kwenye lori hilo kulifunika basi lililokuwa na abiria. Watu 42 waliripotiwa kufariki dunia papo hapo na 23 kujeruhiwa vibaya.

CHANZO: NIPASHE

No comments: