Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Dk. Willibrod Slaa, jana alitinga katika ofisi za Jeshi la
Polisi Kanda ya Dar es Salaam na kutumia saa 6:30 kuwasilisha malalamiko
na ushahidi wa jinsi mlinzi wake, Khalid Kagenzi, alivyokuwa
akiwasiliana na baadhi ya viongozi waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na maofisa usalama kupanga mikakati ya kutaka kumuua.
Dk. Slaa aliwasilisha ushahidi huo ikiwa ni siku mbili tu baada ya
Jeshi la Polisi Kanda ya Kinondoni kumuachia Kagenzi ambaye alikuwa
akihojiwa na jeshi hilo kwa takribani siku mbili na baadaye maofisa wa
Chadema waliomkamata na kumpeleka polisi kugeuziwa kibao kwa kuwekwa
rumande hadi sasa.
Katibu Mkuu huyo aliwasili katika ofisi za Jeshi la Polisi Kanda
Maalum ya Dar es Salaam saa 3:30 asubuhi akiwa amefuatana na mawakili
wawili wa Chadema ambao ni John Mallya na Nyaronyo Kicheere. Dk. Slaa aliwasilisha malalamiko yake ambayo alikuwa ameyaandika
kwa maandishi katika kurasa tisa na kufanya mahojiano na Kamanda wa
Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, yaliyodumu kwa takribani
saa sita na nusu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana mara
baada ya kumaliza mahojiano, Dk. Slaa, alisema kufika kwake kituoni
hapo, kulitokana na wito wa Kamanda Kova. “Chadema tuna ushahidi wa kutosha kuhusiana na njama zote za mauaji
hayo, kwa mantiki hiyo basi, sijaitwa polisi kuhojiwa bali kufikisha
yale niliyokusudia,” alisema Dk. Slaa.
Alisema malalamiko aliyoyawasilisha ni kitendo cha baadhi ya
maofisa Usalama wa Taifa kufanya mawasiliano na Kagenzi na kutoa siri
za mikutano ya ndani za chama hicho na kupanga mikakati ya kutaka
kumdhuru. “Mlinzi huyu (Kagenzi), ametumika kama kiungo katika njama za kutoa
siri za ndani za chama na kupanga njama za kutaka kuniua, tumewasilisha
ushahidi tulioufanyia uchunguzi wa kina,” alisema Dk. Slaa.
Kwa upande wake, Mwanasheria wa Chadema, John Mallya, alisema
malalamiko yaliyowasilishwa polisi kupitia Dk. Slaa, yako sahihi, kwani
kitendo cha Usalama wa Taifa kufanya uchunguzi ndani ya chama fulani na
kuwazuia uhuru wa maamuzi yao, ni kosa kwa mujibu wa sheria.
KOVA KUZUNGUMZA LEO
Kova jana hakuwa tayari kuzungumzia kuhusiana na kuhojiwa kwa Dk. Slaa, badala yake alisema atazungumza leo. Jumapili iliyopita, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere
Marando, aliviambia vyombo vya habari kuwa Kangezi amekuwa akitumiwa na
maofisa 22 wa vyombo vya usalama katika miaka miwili iliyopita kufanya
mipango hiyo dhidi ya chama hicho.
Alidai Kangezi amekuwa akitumiwa na maofisa usalama wa vyombo hivyo kupata taarifa nyingi za Chadema na kuwasilishwa CCM. Marando alidai mipango hiyo imegunduliwa na Kitengo cha Usalama wa
Chadema kupitia simu za Kangezi na kwamba ililenga kuiumiza Chadema
kisiasa. Alidai katika hujuma hizo, Kangezi amekuwa akiwasiliana na
mmoja wa vigogo wa ngazi ya taifa wa CCM.
Marando alidai kuanzia Desemba, mwaka jana hadi wiki iliyopita,
Kangezi alikuwa amekwishafadhiliwa Sh. milioni saba kwa ajili ya
matumizi ya mawasiliano ya simu kufanikisha upatikanaji wa taarifa za
Chadema kupitia vikao vyake mbalimbali, ikiwamo Kamati Kuu.
Alidai alipohojiwa na Chama, Kangezi aliwapa kitabu chake cha
kutunza kumbukumbu, ambacho kinaonyesha mawasiliano kati yake na baadhi
ya maofisa wa vyombo vya usalama, aliowataja kwa majina na namba za simu
zao za mikononi. Hadi sasa vijana watatu wa Chadema ambao wanadai kumpiga Kagenzi bado wanashikiliwa na polisi.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment