
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Saidi Mtanda.
Muswada wa Sheria ya Kupata Habari wa mwaka 2015,
utawasilishwa bungeni Machi 27, mwaka huu, huku wadau wakihofia kuwa
kutoshirikishwa kwao kunaweza kusababisha kutungwa sheria za kuathiri
sekta ya habari.
Kwa mujibu wa ratiba ya mkutano wa 19 wa Bunge linaloendelea mjini
Dodoma, muswada huo na mingine, utasomwa kwa mara ya kwanza na hatua
zake zote kwa hati ya dharura. Kwa maana hiyo, muswada huo umeshakamilika na wadau wa habari
hawatakuwa na fursa yoyote ya kushirikishwa kuutolea maoni kwa lengo la
kuuboresha.
Hata hivyo, kuwasilishwa kwa muswada huo kunaweza kuleta furaha au
kiama kwa wadau wa habari hasa kutokana na kwamba wadau
hawajashirikishwa katika kuuandaa kama taratibu na sheria
zinavyoelekezwa. Kulingana na taratibu, kabla ya muswada huo kuwasilishwa Bungeni,
wadau wa habari wanatakiwa kushirikishwa katika mchakato mzima, lakini
katika mchakato wa Muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari wa mwaka
2015, serikali haijafanya jitihada za kushirikisha wadau.
Badala yake, muswada huo uliandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo huku wadau wakilalamikia kutoshirikishwa. Wadau wanahofia kwamba kutokana na kutoshirikishwa, muswada huo
utawaathiri ikiwamo kutungwa kwa sheria inayoweza kuwaathiri wanahabari
ikiwamo kuweka vigezo vya sifa kwa wanataaluma hiyo.
Vile vile, wanahofia kwamba inaweza kutungwa sheria ya kuminya uhuru wa vyombo vya habari. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Saidi Mtanda,
alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kuwa muswada huo ni
moja kati ya kilio cha wadau wa habari nchini ambao unatarajiwa
kuikomboa taaluma hiyo kwa kusimamia masuala yote yanayohusu taaluma
hiyo muhimu duniani.
TEF: SERIKALI INA AJENDA YA SIRI
Akizungumza na NIPASHE jana, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri
Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, alisema kuwasilishwa kwa hati ya
dharura muswada huo inaonekana dhahiri serikali ina ajenda ya siri
isiyovitakia mema vyombo vya habari nchini.
“Inaonekana dhahiri serikali ina ajenda za siri imezificha, muswada
kuwasilishwa kwa hati ya dharura hakuzingatii misingi ya haki na
demokrasia,” alisema Kibanda. Kibanda alihoji sababu za muswada huo kutoletwa kwa wadau huku
akisisitiza ni vyema ungeletwa kwa wadau wausome ili wautolee maoni
sahihi.
Aidha, alisema kwa mtindo huo ni wazi serikali inataka kuendelea
kuvinyima uhuru vyombo vya habari na wananchi haki ya kupata habari.
MCT: HARAKA YA NINI?
Katibu Mkuu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga,
alihoji kwa nini muswada huo uharakishwe kuwasilishwa bila kukusanya
maoni ya wadau, kitu ambacho ni kuwanyima nafasi ya kuusoma na kutoa
maoni yao.
Mukajanga alisema kwa utaratibu wa utungaji wa sheria, muswada huo
unatakiwa uchapishwe katika Gazeti la Serikali kwa siku 21 ili kutoa
nafasi kwa wadau na wananchi kuusoma, hivyo kama haukuchapishwa matakwa
ya msingi yanawekwa pembeni. Aliongeza kuwa, kufanya hivyo ni jambo linaloogopesha na kuhoji:
“Kwa nini kunakuwapo na usiri katika jambo hili na kulipeleka kwa haraka
bila kushirikisha wadau?”
Alisisitiza kuwa MCT bado inaendelea na juhudi za kuwasiliana na Mawaziri husika ili kuhakikisha wanapata nakala za muswada huo. Kajubi alisema walijitahidi kukutana na Mawaziri bila mafanikio huku akisisitiza kuwa wataendelea na jitihada za kupata nakala.
Alifafanua kuwa ingekuwa vyema kama wadau wangeshirikishwa kwa
ukamilifu kwa ajili ya kupitisha muswada wenye mashiko kwa vyombo vya
habari na sekta ya habari kwa ujumla.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment