
Shahidi wa kwanza Inspekta Jacob Swai katika kesi
inayomkabili Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na wenzake wanane wa Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amedai kwamba washtakiwa waliwakashfu
polisi na kukaidi amri ya kuwazuia wasiandamane.
Kadhalika, amedai kuwa pamoja na Jeshi la Polisi kutoa ilani kwa
wanachama hao kwamba watawanyike na kuwazuia wasiandamane, walikaidi na
kulikashfu jeshi hilo kwamba ni vibaraka wa serikali. Swai alitoa madai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Janeth Kaluyenda,
wakati akitoa ushahidi dhidi ya kesi ya kutotii amri halali ya Jeshi la
Polisi na kufanya mkusanyiko usio halali.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Mohamen Salum, alidai
kuwa Oktoba 14, mwaka 2014, saa 12:00 asubuhi, katika kikao cha utendaji
cha kazi chini ya bosi wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi
Kinondoni, alipokea taarifa kwamba Baraza la Wanawake Chadema (Bavicha),
watafanya maandamano isivyo halali kwenda Ikulu ya Tanzania.
Alidai kuwa saa 4:00 asuhubi alipokea taarifa kupitia simu ya upepo
kwamba Bavicha wamekusanyika Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es
Salaam na kwamba wanataka kuandamana na bango kwenda Ikulu. “Nilipofika eneo la tukio na kikosi kazi changu tuliwakuta wenzetu
wakiongozwa na Mrakibu wa Polisi, Tire… afande Tire alikuwa akitoa ilani
kwa wanachama hao zaidi ya 20 walikuwa wamekusanyika eneo la Makao
Makuu Chadema,” alidai na kuongeza:
“Afande alitoa ilani kwamba watu wote waliokusanyika mahali pale
watawanyike ‘ilani ilani … watu wote mliokusanyika mahali hapa
mnaarifiwa na serikali ya Tanzania kutawanyika kwa amani la sivyo
tutamia nguvu’ ndivyo alivyotoa ilani bosi wangu.”
Alifafanua kuwa baada ya amri hiyo washtakiwa pamoja na wanachama
wengine walikaidi na kutoa kashfa kwamba wameitwa Ikulu na rais kwa hiyo
polisi hawana uwezo wa kuwazuia kuandamani. Alidai kwa kuwa maandamano hayo hayakuwa halali, makundi manne
tofauti ya jeshi hilo yaliingiza kazini kuzuia waandamanaji hao na kundi
lake lilifanikiwa kuwakamata mshtakiwa wa pili, tatu na wa sita.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment