Kansela Angela Merkel wa Ujerumani anatazamiwa kushiriki maandamano ya
jamii ya Waislamu leo hii kukuza suala la uvumilivu katika jamii na
kulaani mashambulizi yaliofanywa na Waislamu wa itikadi kali mjini
Paris.
Rais Joachim Gauck atahutubia katika maandamano hayo yatakayoanza saa
moja usiku katika eneo mashuhuri la Lango la Bradenburg mjini Berlin
maandamano yaliyoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu nchini Ujerumani
chini ya beramu "Kuwepo mashirikiano.Ugaidi sio jina letu". Merkel ambaye atakuwepo takriban na baraza lake lote la mwaziri katika
maandamano hayo amelishutumu kundi la siasa kali za mrengo wa kulia
linalojiita Wazalendo wa Ulaya Dhidi ya Kusilimishwa kwa Ulaya au PEGIDA
kwa kifupi na kusisitiza hapo jana kwamba Uislamu ni sehemu ya
Ujerumani. PEGIDA hapo jana iliwavutia waandamanaji 25,000 katika maadanano yake ya
12 ya kila wiki mjini Dresden mji ulioko mashariki mwa Ujerumani ambayo
zamani ilikuwa chini ya utawala wa Kikomunisti. Wafuasi wake waliokuwa
wakipeperusha bendera walibaki kimya kwa dakika moja kutowa heshima zao
kwa wahanga wa mashambulizi ya gazeti la Charlie Hebdo mjini Paris wiki
iliopita.
Vuguvugu la kupinga PEGIDA lapata nguvu
Maandamano yao hayo yalikabiliwa na maandamano mengine
yanayowapinga yaliohudhuriwa na watu 100,000 nchíni kote ambao
wanaishutumu PEGIDA kwa kutumia vibaya kwa faida yao mashambulizi hayo
yaliofanywa na Waislamu wa itikadi kali nchini Ufaransa ambapo
wameelezea kuunga mkono kwao kuwepo kwa jamii ya tamaduni tafauti nchini
Ujerumani. Merkel hapo jana amewashukuru viongozi wa jamii ya Waislamu milioni nne
wanaoishi Ujerumani kwa kulaani kwa haraka bila ya ajizi mauaji
yaliofanyika kwa kutumia jina la dini yao mjini Paris wiki iliopita. Amesema katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari uliohudhuriwa
pia na Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu kwamba Ujerumani inataka
Waislamu waishi kwa pamoja kwa amani na wafuasi wa dini nyengine na
kwamba maandamano ya leo usiku yatatowa ujumbe mzito.
Merkel halazi damu
Merkel na Davotoglu wiki iliopita waliungana na Rais Farncois
Hollande wa Ufaransa na viongozi wengine duniani katika maandamano
makubwa kabisa ya mshikamano mjini Paris kufuatia mauaji ya watu 17
katika ofisi ya gazeti la dhihaka lilitolewalo kila wiki la Charlie
Hebdo na katika tukio la kushikiliwa watu mateka katika duka moja la
Kiyahudi. Katika taarifa yao Baraza la Waislamu na jamii ya Waturuki nchini
Ujerumani wakati wakilani mashambulizi hayo ya Paris wamesema kuzuka kwa
wimbi jipya la ubaguzi na chuki dhidi ya Uislamu katika mitaa ya
Ujerumani kunazidi kuwapalilia wachochezi na magaidi. Maoni yaliyotolewa kwenye mtandao wa gazeti la Spiegel nchini Ujerumani
yamempongeza Merkel ambaye anajulikana sana kwa kutoyalazia damu masuala
nyeti kwa kutowa kauli ya wazi kulaani chuki dhidi ya Uislamu hata kama
anahatarisha kukipotezea wapiga kura chama chake cha kihafidhina.
CHANZO: DW KISWAHILI

No comments:
Post a Comment