Baraza la Seneti la Ufaransa limepiga kura kuunga mkono azimio
linaloitaka serikali ilitambue taifa la Palestina na kuhimiza mazungumzo
yaanze haraka kati ya Israel na Palestina.
Azimio hilo lilopendekezwa na kutetewa na wafuasi wa chama cha
kisoshialisti,walinzi wa mazingira na wale wa chama cha kikoministi cha
Ufaransa na ambalo haliilazimishi serikali kulitekeleza,limepita chupu
chupu kwa sauti 153 dhidi ya 146.Maseneta wa upande wa upinzani wa
kihafidhina UMP na wale wa kiliberali hawakuunga mkono azimio
hilo.Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Israel imewashukuru waliolipinga
azimio hilo ambalo serikali ya Israel inasema "linawapatia risala mbaya
wapalestina."
Kwa maoni ya mwasisi wa azimio hilo,Gilbert Roger "kutambuliwa dola ya
Palestina ni hatua ya mwanzo ya kuanzishwa uhusiano sawia kati ya Israel
na Palestina na sharti pekee la kuanzishwa mazungumzo ya
dhati."Amesisitiza Ufaransa inabidi iukumbushe ulimwengu kwamba ugonvi
kati ya Israel na Palestina si vita vya kidini,bali ni ugonvi wa ardhi.
Upande wa upinzani wa kihafidhina nchini Ufaransa umekumbusha jukumu la
serikali katika kuhimiza mazungumzo ya amani.Seneta Christian Cambon wa
chama cha UMP amesema na hapa tunukuu"Wapalestina wanastahili hali bora
zaidi kuliko kutambuliwa karatasini.
Juhudi za Nchi za Ulaya kuyafufua Mazungumzo ya Amani
Katibu wa dola anaeshughulikia masuala ya Umoja wa ulaya Harlem
Désir amekumbusha Ufaransa iko tayari kuitisha mkutano wa kimataifa na
pindi juhudi hizo zikishindwa,Ufaransa itabidi iwajibike na kuitambua
dola ya Palestina.
Juhudi hizi za vyama vya mrengo wa shoto vya Ufaransa zinaambatana na
juhudi jumla zinazoendeshwa barani Ulaya wanasiasa wakiamini kwamba
kutambuliwa dola ya Palestina ni njia mojawapo ya kushinikiza
kuendelezwa juhudi za amani zilizokwama na kwa namna hiyo kuuokoa mpango
wa kusaka ufumbuzi wa madola mawili.
Wabunge wa Ireland pia walipiga kura jumatano iliyopita mswaada wa
azimio unaoitaka serikali yao iitambue dola ya Palestina,uamuzi
uliofuatia ule wa mabunge ya Uengereza na Uhispania.
Kura katika baraza la Seneti la Ufaransa imefuatia aile ya disemba 2 iliyopita katika bunge la Ufaransa.
John Kerry aingia tena Mbioni kuuokoa Utarataibu wa Amani
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry alipokutana na
waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu january pili mwaka 2014 nchini
Israel. Wakati huo huo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John
Kerry anatarajiwa kukutana na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
jumatatu ijayo kuzungumzia "mapendekezo kadhaa" pamoja na kuzidi
kuongoezeka idadi ya nchi zinazoushinikiza Umoja wa Mataifa upitishe
hatua katika suala la mzozo wa Israel na Palestina.
CHANZO: DW KISWAHILI
No comments:
Post a Comment