Social Icons

Pages

Wednesday, December 31, 2014

PHIRI KIZUNGUZUNGU SIMBA

Kocha mkuu Mzambia, Patrick Phiri.
Kikosi cha Simba kinaondoka Dar es Salaam leo kwenda Zanzibar kushiriki Kombe la Mapinduzi kikiwa chini ya kocha msaidizi Seleman Matola.

Ingawa uongozi wa Simba bado haujaweka wazi kuhusu kutimuliwa kwa kocha mkuu Mzambia Patrick Phiri, Matola aliiambia NIPASHE jijini Dar es Salaam jana kuwa uongozi umemkabidhi timu kwenda nayo Zanzibar na kumpa jukumu moja tu la kuhakikisha anarudi na kikombe. Endapo timu itarejea jijini bila kikombe, Matola alisema atakuwa amekalia kuti kavu ndani ya kikosi hicho cha Msimbazi, lakini mchezaji huyo wa zamani wa Simba ameahidi kupambana ili kuleta ubingwa wa michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya tisa tangu ianzishwe.
Imeelezwa kuwa kocha mpya Mserbia Goran Kapunovic anatarajiwa kutua jijini leo au kesho kusaini mkataba wa kuifundisha klabu hiyo na taarifa zinaeleza kuwa atasaidiwa na Mnyarwanda Jean Marie kama Matola akichemsha Zanzibar. Katika mahojiano na NIPASHE jijini jana kuhusu usalama wa ajira ya Phiri Simba, Makamu wa Rais wa klabu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema: "Sijui chochote kuhusu suala hilo."
Alipotafutwa na gazeti hili jana mchana, Phiri alisema hajaambiwa chochote na uongozi wa Simba kuhusu nia ya kuvunjwa kwa mkataba wake. "Mimi na Simba ni kama ndugu, ajira zipo lakini sijaambiwa chochote kuhusu kuvunjwa na uongozi, nitawasiliana na Rais (Evans Aveva)," alisema kocha huyo aliyetua nchini kwa mara ya tatu Agosti mwaka huu kuinoa timu hiyo. Hata hivyo, taarifa zaidi kutoka ndani ya uongozi wa Simba zinadai kuwa kulitokea mabishano miongoni mwa wajumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo juu ya uamuzi wa kumtimua hadi wakafikia hatua ya kupiga kura usiku wa kuamkia jana.
Phiri aliyesaini mkataba wa mwaka mmoja kuinoa Simba Agosti 14, mwaka huu akioongoza katika mechi 22 (ameshinda nane, moja ya ligi kuu, sare tisa na kufungwa tano), anakuwa ni kocha wa 18 kutodumu Simba ndani ya miaka 16 tangu 1998 vurugu za kutimua ovyo makocha zilipoanza katika klabu hiyo ya Msimbazi. Kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar katika mechi yao ya raundi ya nane ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwenye Uwanja wa Taifa jijini inaonekana kama sababu kubwa ya kutimuliwa kwake.

OKWI, SSERUNKUMA WAKO UGANDA
Katika hatua nyingine, Matola alisema jana kuwa kikosi chake kinakwenda Zanzibar bila nyota wao Waganda Emmanuel Okwi, Juuko Murushid na Simon Sserunkuma. Simba chini ya Phiri, aliyeiongoza katika mazoezi ya jana asubuhi licha ya kuenea kwa taarifa za kutimuliwa kwake, amekuwa na msimu mgumu katika ligi kuu akitoka sare sita, kipigo kimoja na ushindi mmoja katika mechi nane, hivyo kuwa na pointi 9 katika nafasi ya 10 ya msimamo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: