Mjane wa Mandela, Graca Machel (kushoto) akiwa na shada la mauwaWananchi wa Afrika Kusini leo (05.12.2014) wanakumbuka mwaka mmoja tangu alipofariki dunia Nelson Mandela, rais wa kwanza mweusi nchini humo baada ya kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi.
Kabla ya kuweka mashada ya maua, mjane wa Mandela, Bibi Graca Machel alisema mwili wa Mandela haupo duniani, lakini roho yake haiwezi kubadilika kamwe na itaendelea kubaikia hivyo daima. Amesema anajua kuwa Mandela anafuraha huko aliko, kwa sababu yeye ni miongoni mwa familia aliyochagua kuijenga.
Makamu wa Rais kuongoza dakika tatu za ukimya
Baadaye wananchi wa Afrika Kusini watapuliza vuvuzela, huku honi za magari zikipigwa na kengele zikigongwa kwa dakika tatu na sekunde saba na kufuatiwa na dakika tatu za kukaa kimya, zitakazoongozwa na Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa. Dakika hizo sita na sekunde saba ni kwa ajili ya heshima ya miaka 67 ya utumishi wa umma wa Mandela.
Wananchi wa Afrika Kusini pia wamekuwa wakitafuta njia mbalimbali za kumkumbuka na kumuenzi Mandela, aliyeiondoa nchi yao kwenye giza. Baadhi yao wamekuwa wakijichora tattoo mwilini, ambapo maeneo maalum ya kuchorea tattoo yamekuwa yakifurika watu.
Tutu awasihi wananchi wa Afrika Kusini
Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Askofu Mkuu Mstaafu Desmond Tutu, amewataka Waafrika Kusini kuiga mfano wa Mandela wakati wanapoadhimisha kumbukumbu yake. Amesema wajibu wao kwa Mandela ni kuendelea kuijenga jamii ya haki za binaadamu aliyoiacha.
Baada ya kuachiwa huru kutoka gerezani mwaka 1990, Mandela alitafuta maridhiano ya kutaka kuwepo Afrika Kusini mpya itakayowafanya watu weusi na weupe kuishi kwa kuzingatia haki sawa. Baada ya utawala wa kibaguzi uliodumu kwa miaka 46 kuanguka, Mandela alishinda urais katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia uliofanyika mwaka 1994 na hivyo kuwa rais wa kwanza mweusi, ambapo alihudumu kwa kipindi cha miaka mitano.
CHANZO: DW KISWAHILI

No comments:
Post a Comment