Pages

Wednesday, December 17, 2014

DK. MENGI ALAANI TAARIFA ZA VIGOGO KUMCHAFUA

Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, amelaani taarifa zinazodaiwa kusambazwa na vigogo watatu wa serikali kwamba aliwahonga wabunge mabilioni ya shilingi ili wapinge wizi wa zaidi ya Sh. bilioni 300, uliofanyika katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kuziita kuwa ni za uwongo.
Vigogo wanaodaiwa kusambaza taarifa hizo, wametajwa kuwa ni pamoja na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele; Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakim Maswi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, Dk. Mengi alisema hayo kupitia taarifa yake, aliyoitoa kwa vyombo vya habari, jijini Dar es Salaam jana.
“Hivi karibuni Mheshimiwa Stephen Masele, ambaye ni Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini na Eliakim Maswi, ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo hiyo, wamekuwa wakisambaza taarifa za uongo kwamba mimi nilipeleka mabilioni ya shilingi kwa Mheshimiwa Christopher Ole Sendeka awahonge wabunge wenzake wa CCM ili waweze kupinga vikali wizi wa fedha za umma katika akaunti ya Tegeta Escrow. Huu ni uongo mtupu,” alisema Dk. Mengi. Sendeka ni Mbunge wa Simanjiro kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).Dk. Mengi alisema Sendeka ni rafiki yake, hivyo alimuuliza kuhusu taarifa hiyo.
Alinijibu kwamba siku moja akiwa amekaa meza moja na Mheshimiwa Masele kule Dodoma, alipigiwa simu na kijana wake. Ikabidi aombe radhi na kusogea pembeni ili aweze kusikiliza simu hiyo,” alisema Dk. Mengi. Aliongeza: “Aliendelea kusema kwamba Mheshimiwa Masele ni mtu wa ajabu sana, kwani alimtuma mhudumu eti aje kusikiliza mazungumzo yake ya simu.” Alisema pamoja na kwamba, hilo halikumfurahisha, hakujali kwa sababu alikuwa haongei jambo baya.
Dk. Mengi alisema Sendeka alimwambia pia kwamba, kijana wake huyo jina lake la kwanza ni Reginald kama lake, hivyo kumfanya Masele afikiri kuwa anaongea naye (Dk. Mengi). “Kutokana na maelezo hayo ya Mheshimiwa Ole Sendeka, ni wazi kwamba, mazungumzo aliyoibia Mheshimiwa Masele hayakuwa kati yangu na Mheshimiwa Ole Sendeka na haionyeshwi kwa namna yoyote kuwa yalihusu waheshimiwa wabunge kuhongwa fedha zozote kutoka kwangu kupitia kwa Mheshimiwa Ole Sendeka. Alikuwa na nia mbaya ya kusambaza uongo juu yangu,” alisema Dk. Mengi. Alisema Ijumaa ya Desemba 12, Maswi naye alidai kuwa walirekodi mazungumzo hayo kati yangu na Sendeka.“Kama kweli wanayo rekodi hiyo kama wanavyodai, basi waitoe hadharani,” alisema Dk. Mengi.
Aliongeza: “Kinyume cha hapo, itakuwa jambo la kiungwana kwa Mheshimiwa Masele na Bwana Maswi kufuta matamshi yao ya uongo.” Alisema pia Waziri Wasira katika madai yake alisema anao ushahidi kwamba, Dk. Mengi aliwashawishi wabunge kupinga vikali wizi wa fedha za umma kwenye akaunti ya Tegeta Escrow. Dk. Mengi alisema Waziri Wasira alisema kuwa yeye (Dk. Mengi) alifanya hivyo ili kufanikisha mpango wake wa kuiangusha serikali. “Huu ni uzushi, ambao hauna hata chembe ya ukweli. Nataka Mheshimiwa Wassira atoe ushahidi huo hadharani, la sivyo afute kauli zake za uongo,” alisema Dk. Mengi.
Aliwashauri Watanzania wenye nia mbaya na wenye kusambaza uongo, kumrudiae Mungu na kufahamu kwamba, hatimaye ukweli pekee ndiyo utajidhihirisha na kuwaweka huru.“Wasipofanya hivyo ijulikane kwamba, watakuwa wanadharau na kuchezea zawadi kubwa ya amani na utulivu aliotupa Mwenyezi Mungu,” alisema Dk. Mengi. Aliwasihi viongozi wa madhehebu yote ya dini kusaidia jambo hilo ili Watanzania wote watambue kwamba, ukweli unampendeza Mungu na kudumisha amani ya nchi, lakini uongo unamchukiza Mungu na unaweza kuteketeza taifa. Maswi alipoulizwa na NIPASHE kuhusiana na suala hilo, alikataa kuzungumza, badala yake alimtaka mwandishi akamuulize Dk. Mengi taarifa hizo.
Wasira alipoulizwa alisema hawezi kutoa ushahidi kwa kitu, ambacho hajawahi kukisema.“Nimesema siwezi kuhangaika kutoa ushahidi kwa jambo ambalo sijawahi kulisema na wala halijawahi kuchapishwa. Namuomba Mengi aachane na mambo hayo,” alisema Wasira. Masele hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo na hata alipopigiwa simu zake zote zilikuwa zikiita bila kupokelewa. Jitihada za kumtafuta zinaendelea.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment