Social Icons

Pages

Wednesday, November 19, 2014

WAFANYAKAZI TRA WAFUKUZWA KAZI KWA UDANGANYIFU

Watumishi watano kati ya tisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma ya kuandika taarifa zisizo sahihi juu ya mali zilizokuwamo ndani ya baadhi ya makontena wamefukuzwa kazi.
Akizungumza bungeni jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF), Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema utaratibu wa utoaji wa mizigo bandarini yaani ‘Direct Release’ ulihakikiwa Machi 2013 na kuonekana kuwa na dalili ya kutumika vibaya kwa baadhi ya waagizaji wa bidhaa na makampuni ya mawakala wa forodha.
Alisema kutokana na hali hiyo, TRA waliamua kufanya ukaguzi wa baadhi ya mizigo iliyotiliwa shaka ambapo ilibainika kuwa makontena 270 kati ya 546 yaliyokaguliwa kati ya Aprili na Juni yalikutwa na makosa mbalimbali.
“Uhakiki uliofanyika katika kipindi hicho ulibainisha kuwa jumla ya watumishi tisa walihusika na udanganyifu wa kuandika taarifa ambazo si sahihi juu ya mali zilizokuwamo ndani ya baadhi ya makontena,” alisema.
Aidha, alisema baada ya mamlaka ya nidhamu ya TRA kujiridhisha na taarifa za uchunguzi, ilichukua hatua ya kuwaondoa kazini watumishi watano na watumishi wanne waliobaki walikutwa hawana hatia.
Alisema katika zoezi hilo la uhakiki wa mawakala wa forodha tisa walibainika kuhusika na udanganyifu huo na kwa mujibu wa Sheria ya Forodha ya Mwaka 2014, mawakala hao walifutiwa leseni zao.
Mwigulu alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge huyo aliyehoji ni wafanyakazi wangapi wa TRA wamebainika kujihusisha na udanganyifu wa bidhaa zilizomo ndani ya makontena katika Bandari ya Dar es Salaam.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: