Pages

Thursday, October 23, 2014

SERIKALI IMEKOSA UONGOZI WA PAMOJA?

Rais KIkwete akizungumza na viongozi wa Serikali.

Kwa mshangao mkubwa, tunashuhudia maofisa wa Serikali wakiendelea kutoa kauli zinazokinzana kila kukicha.
Haijapata kutokea tangu nchi yetu ipate uhuru watendaji wakuu serikalini kutoa kauli zinazopishana na kukinzana, tena katika masuala mazito ya kitaifa yanayohusu mustakabali wa nchi yetu.
Inavyoonekana sasa ni kuwa, pengine mkanganyiko uliomo ndani ya Serikali ya Awamu ya Nne ni matokeo ya kukosekana kwa uongozi wa pamoja.
Tunazungumzia hapa kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi waandamizi serikalini kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa, ikiwa ni pamoja na tarehe ya kufanyika Kura ya Maoni kuhusu ‘Katiba Inayopendekezwa’,
 Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uboreshwaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura. Inasikitisha kuona ndani ya Serikali kila mmoja anasema lake kama vile hakuna utaratibu wa kufanya uamuzi wa pamoja kuhusu masuala hayo.
Kwa mfano, kauli iliyotolewa juzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema kwamba Kura ya Maoni itafanyika Machi 30 mwakani na kwamba upigaji kura utatanguliwa na kampeni ambazo zitafanyika kwa siku 30 kuanzia mwanzoni mwa Machi imewashtua watu wengi.
Tunasema hivyo kwa kuwa ameitoa wakati akijua kwamba tayari mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva ametangaza kwamba Tume yake haitaendesha uchaguzi wa aina yoyote, ukiwamo wa Kura ya Maoni hadi uboreshaji wa Daftari la Wapigakura utakapokuwa umekamilika.
 Jaji Lubuva alisema wiki mbili zilizopita kwamba kuendesha chaguzi bila kwanza kuboresha Daftari hilo ni kuongeza malalamiko kutoka kwa wananchi na wadau wengine, vikiwamo vyama vya siasa.
Mkanganyiko unaotokana na misimamo hiyo ya AG na kiongozi wa NEC ni kwamba viongozi hao wanakubaliana kwamba Kura ya Maoni ifanyike baada ya Daftari hilo kuboreshwa. Maswali yanayojitokeza ni kuwa, kama AG anatambua hilo, inakuwaje apange kwamba tarehe ya kufanyika kwa kura hiyo ya maoni ni Machi 30 mwakani, huku akijua msimamo wa NEC ni kwamba uboreshaji wa Daftari hilo hautakamilika hadi Mei mwakani?
 Inakuwaje aseme kampeni zitafanyika kuanzia mwanzoni mwa Machi, huku akijua Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inataka muda huo itolewe elimu ya uraia kati ya miezi mitatu hadi sita kabla ya kufanyika kwa kura hiyo ya maoni?
Sheria hiyo imetoa jukumu hilo la utoaji wa elimu hiyo kwa NEC, hivyo AG anapozungumzia kampeni wakati huo anazidi kuwapotosha na kuwachanganya wananchi. Hiyo inatukumbusha kauli ya Waziri Mkuu katika Bunge la Katiba kwamba Kura ya Maoni ifanyike kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, huku Rais Jakaya Kikwete akisema ifanyike baada ya uchaguzi huo ili kutoa nafasi ya uboreshaji wa Daftari la Wapigakura.
Wakati huohuo, Rais Kikwete alisema hivi karibuni kwamba Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ufanyike Februari mwakani, lakini Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akatangaza baadaye kwamba uchaguzi huo utafanyika Desemba mwaka huu.
Lakini wakati mambo hayajawekwa sawa, jana Rais Kikwete akiwa ziarani nchini China, alitangaza kwamba Kura ya Maoni itafanyika Aprili mwakani.
Kauli hizo zimezidi kuwachanganya wananchi. Sisi tunasema unahitajika uongozi wa pamoja ndani ya Serikali. Nchi inapokuwa na viongozi ambao kila mmoja anatoa kauli inayokinzana na ya mwenzake, matokeo yake ni mfarakano ambao hakika hauwezi kuleta umoja na mshikamano katika kusimamia sheria za nchi na kuwaletea wananchi maendeleo.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment